Papa Francis aonya machafuko Mashariki ya Kati
16 Mei 2018Watu hao waliuawa walipokuwa wakiandamana kupinga kuhamishiwa kwa ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem, uamuzi ulioungwa mkono na taifa la Guatemala ambalo limefuata nyayo hizo za Marekani.
Papa Francis ametoa kauli hiyo wakati wa ibada yake ya kila wiki mjini Vatican, akitoa wito wa mazungumzo, haki na amani. Papa amesema vita inachochea vita na vurugu huchochea vurugu.
" Nina wasiwasi na kuumizwa na kuongezeka kwa mvutano katika ardhi takatifu na mashariki ya kati na kuibuka kwa vurugu ambako kuna sambaratisha amani na majadiliano" alisema Papa.
Israel imekuwa chini ya shinikizo la kimataifa baada ya majeshi yake kuwaua kwa risasi waandamanji 60 a kipalestina katika mpaka wa Gaza walokuwa wakipinga uamuzi wa Marekani wa kuhamishia ubalozi wake mjini Jersalem siku ya jumatatu kutoka Tela Aviv.
Karibu wapalestina wengine 2400 walijeruhiwa katika kile kinachoelezwa kuwai umwagaji mkubwa zaidi wa damu katika mgogoro wa Israel na Palestina tangu vita vya Gaza mwaka 2014.
Papa Francis ameelezea mara kadhaa kuunga mkono ufumbuzi wa mataifa mawili katika mgogoro wa pande mbili, na kumkosoa rais Donald Trump kwa kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.
Hadhi ya mji wa Jerusalem ni mwiba katika mgogoro huo wa wa miongo 7, ambapo Israel inadai mji huo wote mtakatifu kuwa mji mkuu wake, wakati Wapalestina wanataka eneo la mashariki kama mji mkuu wa taifa lao la baadae. Israel ilikalia ukingo wa magharibi na Jerusalem mashariki wakati wa vita ya siku sita mwaka 1967, na baadae kutwaa eneo la mashariki la mji katika hatua ambayo haitambuliwi na jumuiya ya kimataifa.
Guetemala imekuwa nchi ya kwanza kufuata nyayo za Marekani kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem hii leo Jumatano.
Mataifa mengi yamelaani hatua hiyo ya Marekani kama inayodhoofisha uwezekano wa mazungumzo ya amani baina ya Israel na Palestina. Rais wa Guetemala Jimmy Morales amesema kuwa, "Hakika hizi ni enzi mpya ambazo zinatuongoza kufikiri kwamba tutafanya kazi pamoja kwa karibu, kuungana mkono katika njia yoyote na lolote tunaloweza. katika mahusiano baina yetu tunahitaji kusaidiana popote inapowezekana".
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemsififu rais huyo akisema si kwa bahati tu kwamba Guatemala inafungua ubalozi wake Jerusalem ikiwa ni miongoni mwa nchi za kwanza, lakini imekuwa siku zote miongoni mwa watu wa kwanza. Guatemala ilikuwa nchi ya pili kuitambua Israel mwaka 1948.
Paraguay nayo imepanga kuhamisha ubalozi wake mjini Jerusalem baadae mwezi huu. Afisa wa ngazi ya juu wa serikali mamlaka ya Wapalestina katika ukingo wa magharibi Saeb Erekat amesema Guatemala imechagua kusimama upande usio faa na kwamba hatua zitachukuliwa.
Mapema mwezi huu wakati alipoitembelea Venezuela rais wa palestina Mahmoud Abbas aliyotolea mwito mataifa ya Amerika Kusini kutohamisha balozi zake mjini Jerusalem.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi /afp/dpa
Mharirui: Daniel Gakuba