1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis asihi usitishwaji vita Syria mara moja

12 Oktoba 2016

Ndege za kivita za Urusi zimerejelea mashambulizi mazito ya angani katika ngome ya waasi Aleppo na kuua watu 25, miongoni mwao watoto 5. Papa Francis ataka usitishwaji vita ili raia na watoto waondolewe.

Vatikanstaat Heiligsprechung Mutter Teresa durch Papst Franziskus
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Carconi

Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis ameyasihi makundi yanayopigana nchini Syria kusitisha vita mara moja. Wito wa Papa unajiri kufuatia mashambulizi makali yanayofanywa na Urusi hivi sasa mjini Aleppo ambapo watu 25 wameuawa wakiwemo watoto 5.

Mashambulizi mazito ya angani ambayo yamefanywa na Urusi katika ngome za waasi katika maeneo ya Aleppo ndiyo ya karibuni zaidi baada ya siku kadhaa za utulivu kufuatia tangazo la Syria wiki jana kuwa ingelipunguza mashambulizi, ili kuruhusu raia waondoke katika ngome za waasi. Kulingana na kundi moja la kutetea haki za kibinadamu, watu 25 wameuawa miongoni mwao watoto watano. Lakini maafisa wanaotoa misaada ya waokozi wamesema zaidi ya watu 50 wameuawa kufuatia mashambulizi hayo ambayo yamefanywa na ndege za Urusi.

Kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis ameyasihi makundi yanayoshiriki vita nchini Syria kusitisha vita mara moja ili kuruhusu raia waondolewe. Akiwahutubia maelfu ya watu katika uwanja wa Mtakatifu Petero mjini Roma, Papa Francis amesema anatoa wito kwa viongozi kunusuru raia hasa watoto ambao wamezingiriwa katika maeneo yanayoshambiliwa. Papa Francis amesema 

"Ninataka kuangazia na nisisitize ukaribu wangu na waathiriwa wa mashambulizi ya kinyama nchini Syria. Ni kwa haja ya dharura ambapo ninarejelea wito wangu kwa nguvu zangu zote kuwasihi wanaohusika kuyasitisha mashambulizi mara moja, ili kuruhusu raia waondolewe hasa watoto ambao bado wamezingirwa katika maeneo yanayoshambuliwa".

Waokozi wakinusuru waathiriwa wa vita mjini AleppoPicha: picture-alliance/AA/I. Ebu Leys

Mashambulizi hayo yanajiri wakati jamii ya kimataifa ikikumbwa na ghadhabu kuhusu mustakabali wa raia 250,000 ambao bado wapo katika ngome za waasi. Mashambulizi ambayo yanajiri baada ya kuvunjika kwa mkataba wa usitishwaji vita ulioafikiwa kati ya Moscow na Washington.  Suala ambalo limezua mvutano kati ya Urusi na Ufaransa na mataifa mengine huku Marekani ikitangaza kusitisha ushirikiano wake na Urusi kuhusu masuala ya kusitisha vita Syria, nayo Ufaransa ikisema itataka Mahakama ya kimataifa kuichunguza Urusi kwa makosa ya uhalifu wa kivita. Rais wa Urusi Vladimir Putin amekatisha ziara yake iliyotarajiwa wiki kesho mjini Paris baada ya rais wa Ufaransa Francois Hollande kusema atazungumza naye tu kuhusu masuala ya Syria.

Naye waziri wa masuala ya kigeni wa Uingereza Boris Johnson ameyataka makundi ya kuteta haki za kibinadamu nchini mwake kupiga kambi nje ya afisi za ubalozi wa Urusi kama njia ya kuishinikiza Urusi kukomesha mashambulizi mjini Aleppo.

Shirika la uangalizi wa haki za kibinadamu la Syria lenye makao yake makuu London pia limeripoti kuwa waasi pia wamerusha makombora katika shule moja ya msingi kusini mwa mji wa Deraa, na kuua watoto watano. Hata hivyo waasi wamekanusha madai ya kushambulia shule.

Mwandishi: John Juma/RTRE/APE/AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga