1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Papa Francis asubiriwa Timor Mashariki kwa ziara ya kiroho

9 Septemba 2024

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis anatarajiwa kuwasili leo nchini Timor Mashariki kituo cha tatu cha ziara yake ya kuyatembelea mataifa manne ya barani Asia na kanda ya Pasifiki.

Papa Francis
Papa Francis.Picha: Tatan Syuflana/AP Photo/picture alliance

Kwenye mji mkuu wa taifa hilo la kusini mashariki mwa bara la Asia maandalizi ya kumkaribisha Papa Francis yanaendelea ikiwa ni pamoja na usafishaji wa barabara na mamlaka zinawahamisha masikini wanaoishi mitaani.

Waumini wa kikatoliki kutoka maeneo mengine ya nchi hiyo pia wanamiminika kwenye mji huo uitwao Dili kuja kushuhudia ziara ya Papa Francis anayekuwa kiongozi wa kwanza wa kanisa katoliki kuitembelea Timor Mashariki tangu ilipojitangazia uhuru mwaka 2002 kutoka Indonesia.

Akiwa kwenye taifa hilo lenye idadi kubwa ya raia wakatoliki Baba Mtakatifu Francis atafanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa na kidiplomasia na kuongoza misa inayotazamiwa kuhudhuriwa na waumini 700,000.