1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis ataka vita vya Ukraine vikomeshwe haraka

25 Desemba 2022

Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, ametoa wito wa kukomeshwa vile alivyoviita "vita visivyo maana nchini Ukraine" katika ujumbe wake wa Krismasi alioutowa akiwa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Papst Franziskus I Weihnachtsbotschaft „Urbi et Orbi"
Picha: Yara Nardi/REUTERS

"Mungu atupe ufunuo wa kutoa ishara za dhati za mshikamano kuwasaidia wale wanaoteseka, na azitie nuru nafsi za wale wenye nguvu wanyamazishe mirindimo ya silaha na wakomeshe vita hivi visivyo maana haraka sana," alisema Papa Francis mbele ya maelfu ya watu waliokusanyika kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro siku ya Jumapili (Disemba 25).

Mkuu huyo wa Kanisa Katoliki alitoa hotuba hiyo ya Misa ya Krismasi akiwa kwenye roshani kuu ya Kanisa la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kisha 'kuurehemu' mji huo na ulimwengu mzima, maarufu kama "Urbi et Orbi."

Papa Francis mwenye umri wa miaka 86 alitumia hotuba hiyo pia kutaka pakomeshwe mbinu ya kutumia chakula kama silaha, akitaja jinsi vita nchini Ukraine vilivyowatia kwenye hatari ya njaa watu wote ulimwenguni.

Chakula kisiwe silaha ya kivita

"Tunajuwa kuwa kila vita husababisha njaa na hutumia silaha kama chakula... natuanze na wale wenye nafasi za kisiasa kwa kuwataka wajitolee kukifanya chakula kuwa nyenzo ya amani na sio vita," alisema kwenye ujumbe huo uliorushwa moja kwa moja kupitia televisheni na redio kote duniani.

Walinzi wa Uswisi wakilinda Uwanja wa Mtakatifu Petro kueleka Siku ya ujumbe wa Krismasi.Picha: Yara Nardi/REUTERS

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwezi Februari, Papa Francis amekuwa akitoa ujumbe wa mara kwa mara kuvikosowa vita hivyo na akisaka majadiliano na Moscow.

Hata hivyo, amekuwa akikosolewa na baadhi ya watu kwa kutokujitokeza waziwazi kumkosowa Rais Vladimir Putin kwa kuanzisha vita hivyo, badala yake amejikita tu kwenye kuzungumzia madhara yanayotokana na vita hivyo. 

Mapema mwezi Disemba, Papa Francis alilia hadharani wakati akiongoza sala ya maombi kwa ajili ya "taifa lililo matesoni", Ukraine. 

Kwenye mahojiano yaliyochapishwa mwishoni mwa mwezi Novemba katika gazeto la Jesuit la Marekani, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki mwenye asili ya Argentina aliulaani ukatili wa vikosi vya Urusi nchini Ukraine, kauli ambayo ilisababisha Moscow itowe malalamiko rasmi dhidi yake.

"Jitengeni na anasa za dunia"

Papa Francis akiwabariki waumini kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro.Picha: Vatican/AP Photo/picture alliance

Jioni ya Jumamosi (Disemba 24), Papa Francis aliongoza misa ya kila mwaka ya Mkesha wa Krismasi kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro ambayo ilihudhuriwa na waumini wapatao 7,000, kwa mujibu wa Vatican.

Akiwa kwenye kiti chake cha kutembelea kutokana na maumivu ya goti, Papa Francis aliongoza sala maalum kwa "watoto waliosambaratishwa kwa vita, umasikini na dhuluma" na aliwalilia "wanaume wenye njaa ya madaraka na pesa wanaowameza wapenzi na ndugu zao."

Alitowa wito kwa watu "kuachana na pumbazo la kilimwengu" na kugunduwa maana halisi ya Krismasi" katika zama hizi za "matumizi ya anasa", akitetea kuwepo kwa Kanisa linalowahudumia watu masikini. 

Kiasi cha watu 4,000 walifuatilia misa hiyo kupitia tevisheni kubwa zilizowekwa nje ya Kanisa hilo, huku Wakatoliki bilioni 1.3 duniani wakijitayarisha kuadhimisha uzawa wa Kristo.