1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis atembelea kambi ya maangamizi Poland

Admin.WagnerD29 Julai 2016

Kiongozi Mkuu wa kanisa Katoliki Duniani Papa Francis leo alipita peke yake katika lango lenye maandishi "Kazi inatuweka huru''ambayo ni kauli mbiu iliyotumika na wanazi katika kambi ya maangamizi ya Auschwitz..

Kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis alipotembelea kambi ya mauaji ya Auschwitz nchini Poland.
Kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis alipotembelea kambi ya mauaji ya Auschwitz nchini Poland.Picha: Getty Images/AFP/J. Skarzynski

Huku akiwa ameinamisha kichwa chake Papa Francis alifanya sala kabla ya kukutana na walionusurika na maangamizi hayo ya Holocaust na kuwabusu baadhi yao mbele ya ukuta maalumu ambao manazi waliutumia kutekeleza mauaji hayo.

Miongoni mwa walionusurika na mauaji hayo ambao baba mtakatifu Francis alikutana nao ni pamoja na Helena Dunicz Niwinska, mwanamke mwenye umri wa miaka 101 ambaye alipiga chombo cha muziki cha fidla katika bendi ya Aus-shwits pamoja na watu wengine walionusurika katika maangamizi hayo waliokuwa katika eneo hilo.

Papa Francis awasha mshumaa mbele ya ukuta wa mauti

Papa Francis aliwasha mshumaa mbele ya ukuta huo wa mauti na baadaye kuinamisha kichwa kusali kabla ya kutembelea chumba cha jela alichofungwa kasisi wa kipoland na anayetambulika kama matakatifu Maximillian Kolbe ambaye aliuawa baada ya kuchukua nafasi ya mtu ambaye alihukumiwa kifo.

Papa Francis akifanya sala mbele ya ukuta wa mauti wa mauaji yaliyotekelezwa na wanazi ´nchini PolandPicha: Reuters/D. W Cerny

Ziara hiyo ya Papa Francis inakuja katika kipindi cha maadhimisho ya miaka 75 ya siku ambayo Maximilian Kolbe alihukumiwa kifo.

Papa Francis baadaye anatarajiwa kuongoza misa maalumu kwa ajili ya watu waliouawa katika kambi hiyo wengi wao wakiwa wayahudi ambapo amesema asingependelea kutoa mahubiri na badala yake angependelea kukaa kimya huku akibubujikwa na machozi kama ishara ya kuonyesha machungu aliyo nayo kutokana na matukio hayo ya kikatili.

Baada ya kuwasili nchini Poland jumatano wiki hii ambako ni sehemu ambako Ujerumani yazamani ya wanazi iletekeleza maovu hayo alisema ulimwengu hivi sasa uko sawa katika vita ya tatu ya dunia.

Papa Francis amekuwa akirudia kauli yake ya kulaani matukio ya uhalifu yanayofanywa kwa kusingizia imani za kidini baada ya ulaya kukumbana na matukio kadhaa ya mashambulizi yanayotekelezwa na makundi ya itikadi kali.

Tangu alipochaguliwa katika nafasi hiyo mnamo mwaka 2013 kiongozi huyo mkuu wa kanisa Katoliki duniani amekuwa akijitahidi kuimarisha mahusiano kati ya kanisa Katoliki na jamii ya kiyahudi.

Picha: Reuters/K. Pempel

Kiasi ya watu 200 walikusanyika wakiwemo wazee wazamani wa kipoland wanaojulikana nchini humo kama watu wema ambao walijitolea maisha yao kwa ajili ya kuwasaidia na kuwalinda wayahudi wakati wa kipindi cha mauaji hayo kumsubiria Papa Francis mnamo wakati jua lilipokuwa likianza kuchomoza .

Mkuu wa dini ya kiyahudi nchini Poland Michael Schudrich aliunga mkono kauli ya Papa Francis ya kukaa kimya kwa dakika kadhaa kama ishara ya maombi wakati wa kutembelea kambi hiyo ambako mauaji hayo yalitekelezwa akisema mara nyingi watu wanapokwenda katika eneo hilo la Aus- Shwits wamekuwa wakikaa kimya pia lakini akaongeza kuwa badala yake wanapomaliza kutembelea eneo hilo wanapaswa kuendelea kukemea vitendo vya aina hiyo na vinginevyo vinavyokwenda kinyume na misingi ya haki.

Mwandishi : Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri :Yusuf Saumu :