Papa Francis awasifu mashahidi wa Uganda
28 Novemba 2015Papa ametoa sifa hizo katika ibada ya misa takatifu aliyoiongoza na ambayo imehudhuriwa na maelfu ya watu katika madhabahu ya Namugongo, mahali walipochomwa moto mashahidi hao wakiwa hai.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewasifu mashahidi wa Uganda waliochagua kuyapoteza maisha yao badala ya kuikana imani yao ya kikristu. Papa ametoa sifa hizo katika ibada ya misa takatifu aliyoiongoza na ambayo imehudhuriwa na maelfu ya watu katika madhabahu ya Namugongo, mahali walipochomwa moto mashahidi hao wakiwa hai.
Misa hiyo imefanyika katika siku ya pili ya ziara ya Papa Francis nchini Uganda, ambapo aliwasili jana Ijumaa akitokea Kenya. Mashahidi wa Uganda, 22 wakatoliki na 23 waanglikana, waliuawa kwa amri ya mfalme Manga II kati ya mwaka 1885 na 1887, katika juhudi za kuimarisha ushawishi wake uliokuwa ukikabiliwa na vuguvugu la ukristo lililoongozwa na wamisionari kutoka Bara Ulaya.
''Mashahidi hawa wote waliitunza tunu ya Roho Mtakatifu katika maisha yao na walitoa ushuhuda waziwazi juu ya imani yao kwa Yesu Kristo'', amesema Papa Francis katika ibada hiyo ambayo ilitarajiwa kuhudhuriwa na watu takribani milioni mbili.
Ahimiza unyenyekevu na uadilifu
Uganda ni mojawapo ya nchi tatu za kiafrika anazozizuru Papa Francis katika ziara yake ya siku sita, ya kwanza kufanywa na Papa huyo mwenye umri wa miaka 78 katika bara hilo.
Akizungumza katika Ikulu ya Uganda mjini Entebbe Ijumaa, Francis alisema kipimo cha unyenyekevu wa walimwengu kinatazamwa katika namna wanavyowashughulikia wakimbizi.
Katika Ikulu hiyo Papa alipokelewa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni, pamoja na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir. Msemaji wa makao makuu ya Kanisa Katoliki mjini Vatican Federico Lombardi alisema Papa Francis alihimiza kuwepo kwa amani nchini Sudan Kusini, bila kutoa maelezo zaidi.
Mnamo ziara yake nchini Uganda Papa Francis anatarajiwa kuzungumza juu ya mada ambazo pia alizigusia nchini Kenya: Rushwa, umasikini, na haja ya kuwapa vijana wakristo matumaini mema ya maisha ya baadaye.
Hata mashoga waelekeza matumaini yao kwa Papa
Baada ya ibada ya leo Jumamosi, Papa Francis atafanya mazungumzo na vijana, na kisha atalitembelea shirika la kutoa misaada. Papa huyo hali kadhalika atajumuika na watawa wa kikatoliki, wakiwemo mapadre, masista na wanafunzi wa seminari.
Licha ya upinzani mkali wa kanisa katoliki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, mashoga nchini Uganda pia wanayo matumaini kwamba Papa Francis atatetea haki zao, katika nchi yenye sheria kali dhidi ya ushoga.
Katika maandalizi ya kumpokea Papa Francis, wafanyakazi walihangaika usiku na mchana kuziba mashimo katika barabara finyu inayoelekea Namugongo, na madhabahu ya mahali hapo hali kadhalika yalifanyiwa ukarabati mkubwa. Wanajeshi wa kikosi cha uhandisi walishiriki katika shughuli hizo, wakipanda nyasi na kujenga sakafu.
Papa Francis atahitimisha ziara yake nchini Uganda kesho Jumapili na baadaye ataondoka kuelekea katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/dpae
Mhariri: Caro Robi