1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Papa Francis akemea unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.

9 Septemba 2024

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametowa mwito, hatua zichukuliwe dhidi ya unyanyasaji wa vijana wadogo wanaofanyiwa vitendo vya ulawiti. Wito huo ameutoa wakati wa ziara nchini Timor Mashariki.

Papa Francis akiwa mjini Dili
Papa Francis akiwa mjini DiliPicha: Dita Alangkara/AP Photo/picture alliance

Papa Francis ametowa mwito huo huko Timor Mashariki alikowasili leo katika mwendelezo wa ziara yake kwenye eneo hilo la Asia.

Papa Francis baada ya kuwasili Timor Mashariki alipata fursa ya kuhutubia kundi dogo la maafisa wa nchi hiyo yenye idadi kubwa ya Wakatoliki na ambayo ilitumbukia katika mshtuko mkubwa kufuatia matukio ya unyanyasaji wa kingono uliofanyiwa watoto wengi nchini humo.

Viongozi wa kanisa hilo Timor Mashariki walihusishwa kwenye kadhia hiyo iliyotokea miaka ya hivi karibuni.

Na kwa hivyo Papa Francis katika mambo aliyoyatanguliza kwenye hotuba yake ya mwanzo  mjini Dili aliwataka viongozi wahakikishe wanafanya kila wanaloweza kuzuia unyanyasaji wa aina yoyote na kuwahakikishia amani na afya watoto na vijana.

''Pia tusiwasahau watoto wote na vijana waliovunjiwa haki zao. Mtindo huu umezuka dunia nzima. Sote tunatakiwa kuchukuwa hatua kwa kadri tunavyoweza kuzuia unyanyasaji wa aina yoyote na kuhakikisha watoto na vijana wote wanaishi katika mazingira ya afya na amani,'' alisema Papa Francis.

Papa akiwasili Dili-Timor MasharikiPicha: Gregorio Borgia/AP Photo/picture alliance

Papa Francis hakutaja kisa chochote maalum kuhusiana na suala hilo la unyanyasaji kingono watoto na pia hakukiri juu ya Vatican kubeba dhamana ya visa hivyo.Soma pia: Papa Francis aanza ziara ndefu zaidi ya nje

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yalimtolea mwito kiongozi huyo wa kiroho kulikemea suala hilo katika nchi hiyo ya Timor Mashariki wakati kiongozi huyo akiwa tayari huko nyuma alishakutana na wahanga wa unyanyasaji wa kingono katika ziara zake nchini Ireland na Ureno.

Visa vya ulawiti na ubakaji Kanisa Katoliki,Timior Mashariki

Visa vya hivi karibuni kabisa nchini Timor Mashariki ni pamoja na kile kilichomuhusisha mshindi wa tuzo ya Nobel Askofu Carlos Ximenes Belo, ambaye aliadhibiwa kisirisiri na Vatican kwa madai ya kuhusishwa na unyanyasaji wa kingono kwa watoto wadogo aliyoufanya kwa miongo.

Papa Francis akipokewa mjini DiliPicha: Guglielmo Mangiapane/REUTERS

Mwaka 2022 Vatican iliamuwa kuweka hadharani kuhusu kumuwekea vikwazo Askofu Belo baada ya kufichuka kwamba amezuiwa kusafiri na kuzungumza kwa niaba ya kanisa kufuatia madai aliwalawiti vijana wa kiume huko Timor Mashariki kwa miaka kadhaa hadi alipostaafu na kuhamia nje miaka 20 kabla ya hapo.

Soma pia: Papa, Imamu wa Indonesia waonya dhidi ya uchochezi wa kidiniNchi hiyo imeshuhudia historia iliyosheheni matatizo yaliyotokana na utawala wa muda mrefu wa Wareno, miongo kadhaa ya kukaliwa kwa mabavu na Indonesia na hatimae kura ya maoni iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, iliyoipa fursa nchi hiyo kujitenga na kupata ukombozi chini ya Rais Jose Ramos Horta. Papa akawakumbusha wana Timor Mashariki.

"Timor imepitia mateso makubwa na mitihani. Lakini kutokana na kipindi hicho nchi hii imefanikiwa kusimama tena, na kufuata njia ya amani na mwanzo mpya wenye lengo la kuwa na maendeleo ya kuimarisha maisha ya watu wake na kutambuwa umuhimu wa taifa hili kama rasilimali ya ubinadamu.''

Papa akiendesha misa maalum alipokuwa Papua New GuineaPicha: Mark Baker/AP Photo/picture alliance

Papa Francis alikaribishwa kwa shangwe kubwa katika mji mkuu wa Timor Mashariki, Dili ambako maelfu walijipanga kwenye barabara za mji huo wakipeperusha bendera kumpokea kiongozi huyo aliyekuwa ndani ya gari la wazi likisindikizwa na maafisa usalama.

Kesho Jumanne Kiongozi huyo wa kiroho wa kanisa Katoliki duniani anajiandaa kuongoza misa maalum inayotarajiwa kuvutia zaidi ya nusu ya idadi jumla ya wakaazi wa taifa hilo.