Papa Francis awasili Chile
16 Januari 2018Baba Mtakatifu Francis, alilakiwa na mwenyeji wake Rais wa Chile, Michelle Bachelet baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Santiago jana usiku. Hii ni mara ya kwanza Papa Francis mwenye umri wa miaka 81, kuzuru Chile tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki duniani mwaka 2013.
Rais Bachelet ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba mambo mengi yamebadilika tangu Papa Yohane Paulo wa Pili alipozuru Chile mwaka 1987. Amesema wamekuwa jamii yenye kuzingatia haki, uhuru na kuvumiliana, ingawa bado kukosekana kwa usawa limebakia kuwa suala lenye changamoto.
Ziara hiyo itakayomfikisha hadi Peru, inalenga kuimarisha imani kwenye nchi hizo mbili zenye waumini wengi wa Kikatoliki katika wakati ambapo Kanisa hilo linakabiliwa na kashfa kadhaa za unyanyasaji wa kingono na ambako wasiwasi umeongezeka kuhusu dharau hata miongoni mwa waumini wa Kanisa hilo.
Maelfu ya watu walijipanga katika mitaa kwa ajili ya kumsalimu, huku wakipeperusha bendera za Chile na maafisa wa serikali wamesema kuwa wanatarajia zaidi ya watu 500,000 watahudhuria ibada ya misa ya wazi itakayofanyika leo mjini Santiago.
Raia wengi wa Chile bado wameghadhibika kuhusu uamuzi wa Papa Francis kumteua Askofu Juan Barros kutoka mji wa kusini wa Osorno, ambaye ana uhusiano wa karibu na Padri Fernando Karadima, aliyekutwa na hatia na Vatican mwaka 2011 kwa kuwanyanyasa kingono watoto kadhaa wenye umri mdogo kwa kipindi cha miongo kadhaa.
Hata hivyo, Askofu Barros amekanusha madai ya kumlinda, kumtetea na kujua alichokuwa anakifanya Padri Karadima, lakini raia wengi wa Chile bado hawamuamini. ,Msemaji wa jumuia ya Wakatoliki wanaopinga vitendo vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto katika jimbo la Osorno, Mario Vargas, amesema wanapaswa kuombwa radhi kwa vitendo hivyo.
''Tunaamini ni haki na muhimu sisi kulindwa. Tunastahili kuombwa msamaha. Na kitu cha pili tunamuidhinisha padri katika parokia ya Osorno, ambaye amehusika katika unyanyasaji wa kingono, kama padri mzuri huku akilindwa na Askofu Juan Barros,'' alifafanua Vargas.
Kukosekana kwa uaminifu huo kunamuathiri sana Francis, anaeizuru nchi hiyo yenye watu milioni 17, kwa mara ya kwanza katika wadhifa wa Papa. Aidha, wanaharakati wamemtaka Papa kuzungumzia vitendo vya unyanyasaji wa kingono vilivyofanywa na kasisi huyo. Makundi kadhaa yakiwemo ya wanaharakati yameitisha maandamano ya kupinga vitendo hivyo vya unyanyasaji wa kingono katika Kanisa. Imeelezwa pia jumuiya ya mashoga wanatarajia kufanya maandamano, licha ya ulinzi mkali kuimarishwa.
Katika ziara hiyo, Papa atakutana na wazawa wa taifa hilo na kuzungumzia shida wanazozipata wahamiaji na watu wa jamii ya Mapuche ambao wanateswa. Pia atakutana na wahanga wa utawala wa kikatili wa kijeshi wa Jenerali Augusto Pinochet kati ya mwaka 1973 hadi 1990 pamoja na wafungwa wa kike. Baadae Papa atasafiri kwenda Temuco, kusini mwa Santiago na kwenye mji wa kaskazini wa Iquique, kabla ya kuelekea Peru siku ya Alhamisi.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP
Mhariri: Iddi Ssessanga