1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis awasili Thailand

20 Novemba 2019

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewasili nchini Thailand hii leo kwa ziara ya siku nne ambako anatarajiwa kukutana na viongozi wa taifa hilo na kuongoza ibada takatifu. 

Thailand Ankunft Papst Franziskus in Bangkok
Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

Ziara hii inatizamwa kama yenye lengo la kuimarisha utume kwenye mataifa hayo yenye jamii ndogo ya Kikatoliki na kuzungumzia kuhusu masuala yanayoibua wasiwasi ambayo ni pamoja na usafirishaji haramu wa binadamu na masuala ya amani.

Papa Francis amekaribishwa na maafisa wa ngazi za juu wa Thailand wakati alipowasili katika uwanja wa ndege wa kijeshi ulioko Bangkok majira ya mchana, akitokea mjini Rome. Hata kabla ya kusalimiana na viongozi hao alimkumbatia binamu yake Ana Rosa Sivori, anayefanya umishenari nchini humo tangu miaka ya 1960 na ambaye atakuwa mtafsiri wake akiwa Thailand.

20.11.2019 Matangazo ya Asubuhi

This browser does not support the audio element.

Televisheni zilizorusha moja kwa moja tukio la kuwasili kwa kiongozi huyo wa kidini, zilionyesha makundi ya watu waliokusanyika pambezoni mwa barabara za Bangkok, wakisubiri kwa hamu kumuona. Miongoni mwao alikuwa ni Ichaya Methasate aliyesema "Ninajisikia furaha sana na mwenye kubarikiwa sana kwa kupata fursa hii angalau mara moja katika maisha yangu."

Papa Francis atakutana na viongozi wakuu wa Thailand na jumuiya ya Wakatoliki nchini humoPicha: picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

Papa Francis anatarajiwa kuanza ziara yake kwa mkutano wa dakika 15 na waziri mkuu Prayut Chan-o-cha mapema kesho Alhamisi, na baadae atatembelea hekalu ambako atakutana na kiongozi wa waumini wa Buddha nchini humo.

Thailand kwa kiasi kikubwa inakaliwa na waumini wa Buddha na ina karibu waumini 388,000 tu wa Kikatoliki, miongoni mwa idadi jumla ya watu wapatao milioni 69.

Kesho Jioni Papa Francis atafanya mazungumzo ya faragha na mfalme Maha Vajiralongkorn katika kasri la kifalme mjini Bangkok, kabla ya kuongoza ibada takatifu ya misa kwenye uwanja wa taifa mjini humo.

Papa Francis ni wa kwanza kuzuru Thailand na China, tangu Papa John Paul II(pichani) alipozuru mataifa hayo miaka ya 1980Picha: Getty Images/AFP/F. Monteforte

Siku ya Ijumaa, Papa Francis atakutana na jamii ya Kikatoliki ya nchini Thailand, kuongoza ibada nyingine ya misa na hatimaye Jumamosi ataondoka kuelekea Japan ambako atakuwa na ziara ya siku nne hadi Novemba 27.

Papa Francis ni wa kwanza kuzuru Thailand na Japan tangu Papa John Paul wa 11 alipofanya ziara kwenye mataifa hayo mawili miaka ya 1980.

Papa Francis anatarajiwa kugusia pia kuhusu namna anavyovutiwa na Thailand, hasa kutokana na juhudi za wamisionari wa zamani za kuiingiza imani ya Kikatoliki kwenye taifa hilo la Kibuddha, miongo mingi iliyopita.

Ziara yake ya Japan itakuwa ni kama ahueni kwa kiongozi huyo wa miaka 82. Anakabiliwa na upinzani mpya kutoka kwa Wakatoliki wenye misimamo mikali nchini Marekani, kufuatia matamshi yake wakati akihitimisha mkutano kuhusu Amazon uliomalizika hivi karibuni, pamoja na kashfa mpya ya fedha nyumbani kwake.

Kabla ya kuondoka Vatican waziri wa mambo ya nje Kadinali Pietro Parolin alisema masuala kuhusu mahusiano ya imani tofauti pamoja na utu wa kila mtu huenda yakaibuliwa.

Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki ambaye amekuwa kinara wa vita dhidi ya usafirishaji haramu wa binaadamu katika uongozi wake, anatarajiwa kuliibua suala hilo akiwa Thailand, inayotumiwa kama kotovu cha kusafirisha binaadamu, ajira za kulazimishwa na biashara ya ngono.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW