1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis kukutana na vijana wa Kongo

2 Februari 2023

Kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis anakutana na maelfu ya vijana wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake nchini humo.

DR Kongo | Papst Franziskus in Kinshasa
Picha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Takriban vijana 80,000 wanatarajiwa kukutana na Papa, ambaye analenga kuendelea kusambaza ujumbe wa amani na maridhiano baada ya jana Jumatano kukutana na wahanga wa madhila ya machafuko ya nchini humo.

Maelfu ya vijana walianza kuingia katika Uwanja wa Mashahidi ulioko mjini Kinshasa mapema hii leo tayari kabisa kwa mkutano wa hadhara utakaoongozwa na kiongozi huyo wa kiimani.

Uwanja huo unatarajiwa kufurika vijana kama 80,000 hivi ili kusikia ujumbe utakaotolewa na Papa, aliyeko ziarani barani Afrika.

Karibu asilimia 60 ya watu nchini humo ni vijana wa chini ya miaka 20, hii ikiwa ni kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa. Pamoja na mzozo unaoendelea kuwaathiri vijana, wengi pia hawana ajira. Sheila Magumbu, mmoja ya vijana waliojitokeza uwanjani hapo amesema anatumaini kusikia ujumbe wa amani kutoka kwa Papa Francis, na hasa kwa ajili ya wakazi wa mji wa Goma ulioko mashariki mwa Kongo.

Na kama ilivyo kwa Sheila, wengi wanaamini kwamba huo ndio utakuwa ujumbe mkuu ikiwa ni pamoja na maridhiano miongoni mwa watu wa taifa hilo ambalo mizozo imesababisha mamilioni ya watu kuuawa katika miongo kadhaa iliyopita, huku watu milioni 5.7 wakiwa hawana mahala pa kuishi baada ya kuyakimbia makazi yao.

Baadhi ya wakazi wa Kongo walioshiriki ibada ya misa iliyoongozwa na Papa Francis jijini Kinshasa.Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Hapo jana, Papa Francis alikutana na wahanga wa madhila ya machafuko nchini humo na kusikiliza visa vya kutisha na kusikitisha. Kulingana na vyombo vya habari, Papa alisikiliza kwa umakini mkubwa shuhuda zilizotolewa kuanzia za kijana aliyelazimika kutizama wakati baba yake akikatwakatwa viungo, kisa cha msichana mdogo kubakwa kama mnyama kwa miezi kadhaa na mtumwa wa zamani wa ngono aliyelazimishwa kula nyama za watu.

Kiongozi huyo aliyalaani vikali matukio hayo aliyoyaita uhalifu wa kivita.

Soma Zaidi: M23 wazidi kuteka maeneo mashariki ya Kongo

Na baada ya mazungumzo na Papa, baadhi yao waliviambia vyombo vya habari kwamba hatimaye kuna matumaini makubwa ya amani baada ya kupata fursa hiyo.

Eneo la Mashariki mwa Kongo ndilo hasa limekumbwa na machafuko kwa miongo kadhaa sasa inayochochewa kwa sehemu na mvutano kati ya serikali, waasi na wavamizi kutoka nje juu ya udhibiti wa eneo kubwa lenye hifadhi ya madini.

Soma Zaidi: Papa Francis ayataka mataifa ya kigeni kuacha kuipora Kongo

Papa Francis, anatarajiwa pia kupeleka ujumbe wa amani nchini Sudan Kusini kesho Ijumaa, atakapofanya ziara ya siku tatu kwenye taifa hilo changa kabisa ulimwenguni lakini lililoathiriwa pakubwa na vita vilivyosababisha vifo vya karibu watu 380,000.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW