1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis kuzikwa siku ya Jumamosi mjini Roma

22 Aprili 2025

Shughuli ya kuutazama mwili wa Papa Francis kwa umma itaanza Jumatano wakati ibada ya mazishi ikipangwa kufanyika Jumamosi.

Mwili wa Papa Francis ukiwa kwenye jeneza la wazi
Mwili wa Papa Francis ukiwa kwenye jeneza la waziPicha: Vatican Media/REUTERS

Ulimwengu na waumini wa Kanisa Katoliki kwa ujumla wake wanaendelea kuomboleza kifo cha kiongozi mkuu wa kanisa hilo duniani Papa Francis, aliyefariki siku ya Jumatatu. Makao makuu ya kanisa hilo Vatican, yametangaza kwamba atazikwa Jumamosi katika kanisa la Mtakatifu Maria Mkuu, mjini Roma.

Hivi sasa makadinali wamekutana Vatican kuanza kuweka mipango ya ibada ya mazishi pamoja na kuzikwa kwa kiongozi huyo mkuu wa kiroho wa Kanisa Katoliki duniani, lakini pia kuandaa baraza maalum litakalopiga kura kumchagua atakayemrithi pamoja na kufanya maamuzi mengine kuhusu uendeshaji wa kanisa hilo.

Taarifa zilizotangazwa na Vatikan zinasema kwamba utaratibu wa umma kuanza kuutazama mwili wa Papa Francis utaanza rasmi Jumatano, Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter, huku shughuli za ibada ya mazishi ya kiongozi huyo zikipangwa kufanyika siku ya Jumamosi saa nne asubuhi katika uwanja wa kanisa hilo.

Watu waliojitokeza kuomboleza kifo cha PapaPicha: Martin Cossarini/REUTERS

Picha za kwanza za mwili wa Papa uliolazwa katika jeneza akiwa amevishwa mavazi maalum mekundu na kofia ya kiaskofu na kushikilia Rozari, zimechapishwa leo na kuoneshwa kwa umma huku akionekana kiongozi wa shughuli za kidiplomasia na kisiasa ndani ya Vatican, ambaye anatazamwa kama kiongozi wa juu wa Papa anayesimamia shughuli za Kanisa akiuombea mwili huo katika Kanisa la Mtakatifu Marta alikokuwa akiishi Papa.Soma pia:Mwili wa Papa Francis kuwekwa kanisa la Mtakatifu Marta

Viongozi mbalimbali wa dunia na Wakristo waumini wa Kanisa Katoliki wameendelea kuomboleza kifo cha kiongozi huyo wa kiroho, aliyekuwa wa kwanza katika historia ya kanisa hilo kuchaguliwa papa kutoka kanda ya Amerika ya Kusini. Kuanzia barani Afrika, Asia, Ulaya na kwengineko salamu za rambirambi zimeendelea kumiminika watu wakiukumbuka mchango uliotolewa na Papa Francis.

Soma pia: Tanzia: Papa Francis, mhafidhina aliyependa mabadilikoWafilipino wanamkumbuka kwa roho ya kujali aliyowaonesha wagonjwa na walionusurika majanga ya asili. Mamia ya Wafilipino wamekusanyika leo kwenye misa maalum iliyoandaliwa katika kanisa la mjini Manila huku wakilia na kumuaga buriani Papa Francis ambaye wanamkumbuka pia kwa kujitowa kuwaangalia masikini  na waliokumbwa na majanga ya asili ambayo yamewahi kutokea katika nchi hiyo mara kwa mara,aliyowahi kuitembelea mwaka 2015. Mwadhama Gianfranco Kadinali Ravasi anamzungumzia kama ifuatavyo.

Mishumaa ikiwaka katika kanisa la Mtakatifu PeterPicha: ABACA/IPA Sport/picture-alliance

''Alikuwa papa msikivu kwa masuala yaliyohusu tamaduni za wanawake na matatizo ya vijana, lakini pia sayansi, teknolojia hadi Akili Mnemba na pia naweza kusema alifuatilia masuala yaliyohusu mawasiliano, teknolojia ya kigijitali na zaidi alikuwa mtu aliyeiboresha lugha ya kanisa. Alitumia baadhi ya maneno ambayo yote yalikuwa na mchango mkubwa na kuruhusu watu wajihisi wenye faraja.''

Barani Afrika Papa Francis anakumbukwa kwa moyo wake wa upendo kwa watu wa bara hilo wanaoshuhudia migogoro. Kanisa Katoliki limesema urithi wake anaouacha kuhusu bara hilo ni kiu chake cha kutaka kuona amani, haki ya kijamii na maendeleo kwa bara hilo sambamba na mshikamano wake aliouonesha kwa wakimbizi na wahamiaji wa Kiafrika na watu masikini na waliotengwa katika jamii.

Kuanzia Australia, hadi India bendera zimeteremshwa nusu mlingoti kuomboleza kifo cha Papa. Nchini India bendera zinapepea nusu mlingoti katika majengo yote ya serikali kwa siku tatu kuomboleza na kutowa heshima kwa kiongozi huyo wa kiroho.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW