Papa Francis: Mazungumzo ya Korea yawe ya uwazi
25 Aprili 2018Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, wako mbioni kukutana kwenye kijiji cha mpakani cha Panmunjom siku ya Ijumaa. Papa Francis aliyeizuru Korea Kusini mwaka 2014, amewatolea mwito viongozi hao kuwa na "ujasiri wa matumaini, na hivyo kuwa wajumbe wa amani".
"Mkutano huu utakuwa fursa nzuri ya kuanza mazungumzo ya uwazi na njia thabiti ya upatanishi na ushirika mpya, ili kuhakikisha amani katika rasi ya Korea na duniani kote," alisema Papa Francis.
Kim Jong Un anakutana na mwenzake wa Kusini kabla ya kukutana na Rais Donald Trump wa Marekani wiki chache zijazo. Mkutano wa Ijumaa unakuja baada ya mvutano kushamiri mwaka uliopita wakati Korea Kaskazini ilipozidisha kasi katika kuuendeleza mpango wake uliopigwa marufuku wa silaha za nyuklia, huku Trump pia akianzisha vita vya maneno na kiongozi wa Pyongyang. Mara ya mwisho mataifa hayo kufanya mkutano kama huo ilikuwa ni mwaka 2000 na 2007.
Kamera za baadhi ya vyombo vya habari vikubwa duniani zitarusha picha za moja kwa moja za kiongozi wa Korea Kaskazini ambaye huwa anadhibiti kila kipengele cha mwonekano wake ndani ya nchi hiyo na duniani kote, ingawa haijakuwa wazi ikiwa picha hizo zitaonyeshwa mara moja Korea Kaskazini.
Licha ya tangazo kwamba baadhi ya matukio ya mkutano huo yataonyeshwa moja kwa moja, na uwezekano wa mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari, rais Moon anaonekana kuwa na dhamira ya kumfanya kiongozi wa Korea Kaskazini ajisikie huru na fujo za vyombo vya habari vya ndani, wakati mkutano huo ulitarajiwa kuyavusha mataifa hayo kutoka ukingo wa vita ya mwaka jana hadi katika ushirikiano, ambao Moon amekuwa akiuota.
Mawazo hayo yanaweza kuwa magumu kwa Moon mwenye nia ya kuandika historia na mazingira yatakayo wezesha mkutano baina ya Kim na Trump. Wakati Kim anaweza kushindwa kudhibiti kila kitakachotokea upande wa Korea Kusini, Seoul inaonekana kuwa na hamu ya kuhakikisha mambo yanakwenda barabara, hata kuandaa hafla itakayojumuisha chakula kutoka Uswisi, mahali alikosoma Kim enzi za ujana wake.
Taarifa za mkutano huo huenda zikadhibitiwa kwa kiasi kikubwa isipokuwa tu kwa kundi la waandishi watakaohudhuria mkutano, na ambao kibali chao kinaweza kuwa na mipaka. Kuelekea mkutano huo, rais Moon amekoselewa na vyombo vya habari kwamba serikali yake imewahimiza watetezi maarufu na wachambuzi wa kihafidhina kukaa mbali na vyombo vya habari, kwa kuzingatia kwamba wanaweza kuikasirisha Korea Kaskazini, ambayo inafuatilia kwa karibu mambo hayo, madai ambayo serikali ya Seoul imeyapinga vikali.
Waziri wa mambo ya nje wa Korea ya Kusini Kang Kyung-hwa amesema Seoul haitagusia kwenye mkutano huo madai ya Umoja wa Mataifa ya ukandamizaji wa Kim Jong Un dhidi ya watu wake akisema hilo ni suala linalohitaji maandalizi zaidi.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters/AP/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga