Papa Francis yuko ziarani Uturuki
28 Novemba 2014Ziara hiyo pia imelenga kuhimiza maelewano na Waisilamu na kulaani mauaji ya mateso kwa Wakristo katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kabla ya ziara yake papa Francis alilaani mashambulizi dhidi ya makundi ya watu wachache nchini Iraq, akiyataja kuwa ya kinyama, ya kihalifu na yasiyoelezeka. Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki amewataka viongozi wa kiislamu wajiepushe mbali na vitendo vya aina hiyo.
Vilio vya Wakristo, Wayazidi na jamii nyingine vinadai msimamo ulio wazi na imara kutoka kwa viongozi wa dini wa makundi yote, hususan waislamu na viongozi wa siasa pia, alisema baba Mtakatifu Francis katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la kila siku la Israel, Yediot Ahronota.
Ndege iliyombeba papa Francis iliondoka uwanja wa ndege wa mjini Roma mwendo wa saa tatu na robo leo asubuhi na ilitarajiwa kutua katika uwanja wa ndege a mjini Ankara baada ya muda wa masaa matatu.
Akiwa mjini humo Papa Franscis amepangiwa kukutana na rais wa Uuruki Recep Tayyip Erdogan na waziri mkuu wa nchi hiyo Ahmet Davutoglu. Atalitembelea eneo la makumbusho la Ataturk na Diyanet, chombo cha umma kinachoratibu masuala ya kiislamu.
Hapo jana Erdogan aliashiria hayuko tayari kuambiwa cha kufanya na wageni. Erdogan alisema na hapa namnkuuu, „Wale wanaokuja kutoka nje wanapenda petroli, dhahabu, almasi, nguvu kazi ya gharama ya chini, machafuko, mapigano na mivutano ya kutoelewa katika eneo la Waislamu. Wale wanaokuja kutoka nje wanaweza kuonekana kuwa marafiki katika macho yetu lakini wanapenda maiti zetu na za watoto wetu,“ mwisho wa kumnukuu.
Hapo kesho Baba Mtakatifu Franscis amepangiwa kusafiri kwenda mjini Istanbul kulitembelea jumba la makumbusho la Sophia na msikiti mmoja unajulikana kama Msikiti wa Buluu, Blue Mosque, na kuongoza misa katika kanisa Katoliki mjini humo ambako wakimbizi Wakristo kutoka nchini Iraq wanatarajiwa kuhudhuria.
Ziara yake itakamilika siku ya Jumapili ambapo atasherehekea sikukuu ya Mtakatifu Andrew, mtume wa madhahebu ya Orthodox, pamoja na Bartholomayo, kiongozi wa kiroho wa waumuni milioni 300 wa madhebu ya Orthodox ulimwenguni.
Papa Francis aliyechaguliwa kuliongoza kanisa katoliki mnamo Machi mwaka 2013 ameshaitembelea Brazil, Korea Kusini, Albania na hivi karibuni alifanya ziara mjini Strasbourg nchini Ufaransa. Amepangiwa kuizuru Sri Lanka na Ufilipino kuanzia tarehe 12 hadi 19 Januari mwaka ujao.
Mwandishi: Nyamiti Kayora/DPA/AFP
Mhariri:Josephat Charo