Papa: Kuwanyanyasa wanawake ni uhalifu dhidi ya ubinadamu
20 Machi 2018Papa Francis alitoa kauli yake ya dhati kabisa katika kikao cha kusisimua cha maswali na majibu na vijana kutoka mataifa mbalimbali ya dunia waliokwenda mjini Roma kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa maaskofu uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu katika makao makuu ya kanisa huko Vatican. Jumla ya vijana 300 walialikwa kwenda Vatican wiki hii kuwasaidia viongozi wa kanisa Katoliki kujifunza jinsi vijana wanavyofikiri kuhusu kanisa Katoliki siku hizi.
Papa alisema, "Ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Na unatokana na fikra mbovu kwamba wanawake lazima wadhalilishwe. Hadi leo hakuna kampeni yoyote ya wanawake iliyofanikiwa kulifuta jambo hili kutoka kwa fikra jumla za mwanadamu kwamba wanawake lazima wanyanyaswe."
Papa Francis aliomba msamaha kwa niaba ya wakristo wote wanaonunua ngono kutoka kwa wanawake, akisema wanaume wanaokwenda kutafuta huduma kwa makahaba ni wahalifu wenye fikra mbovu na wanaofikiri wanawake wapo tu kwa ajili ya kunyanyaswa.
Blessing Okoedion msichana wa Nigeria mwenye umri wa miaka 32, na ambaye aliwahi kuwahi kuwa muhanga wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ukahaba, alimuuliza Papa Francis jinsi gani kanisa limewaruhusu waumini kuwa wateja wa wanawake wengi kutoka Nigeria walio nchini Italia kama yeye, wanaolazimishwa kuwa watumwa wa ngono na wafanyabiashara waliowasafirisha kimagendo hadi nchini humo.
"Kinachonisumbua sana ni mahitaji makubwa ya makahaba, idadi kubwa sana ya wateja, wengi wao waumini wa kanisa Katoliki kama ilivyodaiwa. Nashangaa sana na nakukuuliza Baba Mtakatifu. Je, kanisa linaweza kuingilia kati na kutafuta jawabu mujarabu la idadi hii kubwa ya wateja?"
Waumini wa kanisa Katoliki waliobatizwa watuhumiwa
Papa Francis alijibu akisema nchini Italia kuna uwezekano asilimia takriban 90 ya wateja wanaume wanaokwenda kwa makahaba ni waumini wa kanisa Katoliki waliobatizwa.
Makahaba, wengi wao wahanga wa usafirishaji haramu wa binadamu kutoka Nigeria na mataifa mengine ya Afrika na Ulaya Mashariki, huonekana wakati wa usiku katika barabara zilizo nje kidogo ya mji wa Roma na pia katika maeneo yanayoyazunguka mabustani.
Katika mkutano huo wa jana wajumbe 300 katika chuo kikuu cha mjini Roma, Papa Francis alisema unyanyasaji wa ngono dhidi ya wanawake unatokana na fikra mbovu zilizokita mizizi katika akili za watu wengi. Kiongozi huyo aidha aliwataka vijana wapambane na tatizo hili, huku akipinga wazo kwamba kwenda kwa makahaba huenda kusiwe na madhara yoyote.
Papa Francis pia alisikia kauli nzito kutoka kwa Angela Markas, msichana mwenye umri wa miaka 22 kutoka Australia aliyesema kuna mwenendo katika kanisa la kuepuka masuala nyeti ambayo sio rahisi kuyazungumzia, yakiwemo jinsia, ndoa za watu wa jinsia moja, na pia jukumu la wanawake katika kanisa.
Mapema mwezi huu wanawake wa kanisa Katoliki wakiongozwa na rais wa zamani wa Ireland Mary Patricia McAleese walitaka jukumu kubwa zaidi la wanawake katiak mchakato wa kupitisha maamuzi katika kanisa, wakimhimiza papa Francis kuvunjilia mbali kuta zinazowatenga wanawake.
Mwandishi: Josephat Charo/rtre/
Mhariri: Mohammed Khelef