Papa Leo kuanza ziara ya siku 10 katika mataifa 8 ya Afrika
9 Aprili 2026
Kwa mujibu wa Vatican, ziara hiyo ni miongoni mwa vipaumbele binafsi vya Papa Leo tangu achaguliwe mwaka 2025, ikiwa ni safari yake kubwa ya kwanza ya kimataifa mwaka 2026. Katika safari hiyo, atatembelea miji 11 tofauti na kutoa hotuba zaidi ya 25, huku akikutana na viongozi wa kisiasa na waumini wa kanisa.
Maafisa wa Vatican wanasema Papa Leo analenga kuhamasisha viongozi wa dunia kuelekeza nadhari zaidi Afrika, hasa katika kukabiliana na changamoto za migogoro, umaskini na ukosefu wa utulivu wa kisiasa. Aidha, anatarajiwa kuhimiza mazungumzo ya kidini, hasa kati ya Wakristo na Waislamu, hususan nchini Algeria.
Nchini Cameroon, Papa Leo atahudhuria mkutano maalum wa amani katika mji wa Bamenda, eneo ambalo limekumbwa na mzozo wa muda mrefu kati ya serikali na makundi ya wanaotaka kujitenga. Ziara hiyo pia inalenga kuionesha Afrika kama bara lenye matumaini na uwezo wa kustahimili changamoto mbalimbali.
Katika muktadha huo, viongozi wa kidini wanasema ujumbe mkuu wa Papa Leo katika ziara hii ni amani, mshikamano na kuishi kwa pamoja licha ya tofauti zilizopo katika jamii.
Papa Leo kutembelea vituo vya historia ya Ukristo
Ziara hiyo pia itampeleka Papa Leo katika maeneo yenye historia muhimu ya Ukristo, ikiwemo mji wa Annaba nchini Algeria, ambako kuna mabaki ya mji wa kale wa Hippo uliokuwa makazi ya Mtakatifu Augustine, mmoja wa viongozi muhimu wa kanisa la mwanzo.
Fred Wekesa, mkuu wa Basilica ya Mtakatifu Ausgustin alisema kuwa -"anakuja kutuletea ujumbe wa amani na pia kutuhimiza kufanya mazungumzo na kuendelea kuishi kwa amani na kuishi pamoja kwa utulivu, jambo ambalo ni muhimu sana. Kwa sababu kwake, kama alivyosema alipokuwa akitoka Lebanon, amani ni ya muhimu sana na angependa kuendeleza dhamira hii ya kukuza na kuimarisha kuishi pamoja kwa amani na mazungumzo katika maisha, ili tuishi pamoja, kama vile Mtakatifu Augustino alivyotuhimiza kuishi katika jamii kwa umoja na maelewano, tukiwa na nia moja na moyo mmoja chini ya Mungu aliyetuumba sote," alisema Wekesa.
Nchini Angola na Equatorial Guinea, Papa Leo anatarajiwa kuzungumzia masuala ya maendeleo, haki za binadamu na umuhimu wa kuimarisha taasisi za kidemokrasia, huku akitoa faraja kwa jamii zinazokabiliwa na changamoto za kiuchumi na kijamii.
Wachambuzi wanasema ziara hiyo inaweza kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu changamoto zinazoikabili Afrika, lakini pia kuonesha nafasi ya bara hilo kama kitovu cha ukuaji wa Kanisa Katoliki duniani.