1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaAfrika

Ziara ya Papa Guinea ya Ikweta na mtihani wa kidiplomasia

21 Aprili 2026

Papa Leo XIV anaelekea Guinea ya Ikweta, inayoongozwa na Rais wa muda mrefu zaidi duniani, akikabiliwa na changamoto za ufisadi, siasa na matumaini ya mabadiliko katika ziara yake ya Afrika.

Angola, Saurimo 2026 | Papa Leo XIV anaongoza Misa Takatifu
Ziara ya Papa Leo XIV barani Afrika imebeba ujumbe wa amani, matumaini kwa vijana na kupinga ufisadi na matumizi mabaya ya madarakaPicha: Guglielmo Mangiapane/REUTERS

Papa anatarajiwa kuwasili Jumanne nchini Guinea ya Ikweta, ikiwa ni hatua ya mwisho ya ziara yake katika mataifa manne ya Afrika—akiwa anakabiliwa na changamoto nyeti zaidi ya kidiplomasia tangu aanze uongozi wake.

Nchi hiyo ndogo ya Afrika ya Magharibi inaongozwa na rais mwenye muda mrefu zaidi madarakani barani humo, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, mwenye umri wa miaka 83, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1979 na kukabiliwa na tuhuma za ufisadi na utawala wa kimabavu.

Ugunduzi wa mafuta baharini katikati ya miaka ya 1990 ulibadilisha kwa kasi uchumi wa Guinea ya Ikweta. Kwa sasa, mafuta yanachangia karibu nusu ya pato la taifa na zaidi ya asilimia 90 ya mauzo ya nje, kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, AfDB.

Hata hivyo, zaidi ya nusu ya watu karibu milioni mbili wanaishi katika umaskini. Mashirika ya haki za binadamu kama Human Rights Watch pamoja na kesi zilizofunguliwa Ufaransa na Uhispania zimeonyesha kuwa mapato ya mafuta yamenufaisha zaidi familia ya rais kuliko wananchi wa kawaida.

Papa Leo alikaribishwa nchini Angola na Rais Joao Lourenco, Aprili 18, 2026Picha: Guglielmo Mangiapane/REUTERS

Papa akitoa ujumbe mkali dhidi ya ufisadi

Katika ziara yake ya kwanza Afrika kama papa, Leo XIV ameonyesha wazi kuwa hatasita kukosoa. Mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu ukosefu wa usawa na ufisadi yako wazi, na huenda ujumbe wake nchini Guinea ya Ikweta ukawa mkali zaidi.

Akiwa nchini Cameroon wiki iliyopita, alikutana na rais Paul Biya, mwenye umri wa miaka 93—kiongozi mzee zaidi duniani.

Akiwa pembeni ya Biya, papa alisema: "Ili amani na haki vitawale, minyororo ya ufisadi lazima ivunjwe… mioyo lazima iachane na tamaa ya mali kupita kiasi.”

Kauli hiyo inaashiria kuwa huenda akatoa ujumbe kama huo pia nchini Guinea ya Ikweta.

Ingawa Guinea ya Ikweta ni nchi ya kidunia, Kanisa Katoliki lina nafasi kubwa katika mfumo wa kijamii na kisiasa. Takriban asilimia 75 ya wananchi ni Wakatoliki.

Mwanaharakati Tutu Alicante anaeleza kuwa uhusiano kati ya serikali na viongozi wa kanisa ni wa karibu sana: "Kuna hofu iliyojengwa na serikali, lakini pia kuna manufaa ya kifedha ambayo kanisa hupata.”

Kwa upande mwingine, Fortunatus Nwachukwu kutoka Vatican anasema kanisa lazima lisawazishe kati ya kuikosoa serikali na kuendelea kutimiza wajibu wake wa kiroho: "Kanisa haliwezi kupigana vita na serikali, lakini pia haliwezi kukubali kila kitu kama kilivyo.”

Makadinali waanza kumchagua Papa

01:24

This browser does not support the video element.

Tuhuma za ukandamizaji na ufisadi sugu

Mbali na ufisadi, serikali ya nchi hiyo inakabiliwa na tuhuma za kukandamiza wapinzani, wanaharakati na wanahabari.

Kwa mujibu wa Transparency International, nchi hiyo mara nyingi huorodheshwa miongoni mwa nchi 10 za mwisho duniani kwa kiwango cha ufisadi.

Mshauri wa shirika hilo barani Afrika, Samuel Kaninda, anasema hatua za kupambana na ufisadi zimeanza kuchukuliwa, lakini mafanikio yake yatategemea uhuru wa taasisi husika.

Anaamini ziara ya papa inaweza kuongeza shinikizo la mageuzi na kuwapa matumaini wananchi: "Kuna hatari ya kisiasa, lakini pia ni fursa ya kuangazia kinachoendelea nchini humo.”

Matumaini na fursa kwa wananchi

Ziara ya papa nchini humo ni ya kwanza tangu ile ya John Paul II mwaka 1982.

Atakapowasili, atakutana na rais Obiang na kutoa hotuba kwa viongozi wa serikali na wanadiplomasia, kisha atahutubia katika chuo kikuu cha taifa.

Ratiba yake pia inajumuisha: Kuongoza misa; Kutembelea hospitali ya wagonjwa wa akili; Kutembelea gereza; Kukutana na vijana na familia zao.

Kabla ya kuondoka Alhamisi, ataomba katika kumbukumbu ya waathirika wa mlipuko wa mwaka 2021 katika kambi ya jeshi mjini Bata uliosababisha vifo vya zaidi ya watu 100.

Kwa baadhi ya wananchi, ziara hiyo tayari imeleta manufaa ya kiuchumi. Fundi cherehani Tumi Carine anasema: "Ujio wa papa umetuletea wateja wengi… tunashukuru sana.”

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW