1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Leo XIV ahimiza kugawa kwa haki maliasili za Afrika

Zainab Aziz DPA/RTRE/AFP
20 Aprili 2026

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo XIV ametoa wito wa kugawanywa kwa haki maliasili za barani Afrika alipoongoza Misa iliyohudhuriwa na watu wapatao 60,000 katika jiji la Saurimo.

Angola Saurimo 2026 | Papa Leo XIV
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo XIV alipotembelea nyumba ya kuwalea wazee katika mji wa Saurimo nchini Angola Picha: Vatican Media/Catholic Press Photo/IMAGO

Saurimo ni mji mkuu wa jimbo la Lunda Sul lililokuwa limetengwa kihistoria lililo karibu na mgodi mkubwa zaidi wa almasi nchini Angola, Catoca, ambako huchimbwa takriban asilimia 75 ya almasi nchini humo.

Angola ina utajiri mkubwa wa malighafi, na pia ni muuzaji wa mafuta na gesi. Hata hivyo, wengi kati ya wakazi wake milioni 37 bado wanaishi katika umaskini kutokana na athari za muda mrefu za mgogoro huku kukiwa na pengo kubwa la usawa kati ya matajiri na maskini.

Papa Leo XlV katika ziara kwenye mji wa Saurimo nchini AngolaPicha: Vatican Media/Catholic Press Photo/IMAGO

Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miongo kadhaa baada ya Angola kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Ureno mnamo mwaka wa 1975, majeshi na vikundi mbalimbali vya waliomiliki silaha vilifadhiliwa kwa mapato yaliyotokana na biashara ya almasi na mafuta.

Angola ni kituo cha tatu katika ziara ya Papa Leo, barani Afrika. Kiongozi huyo mkuu wa Wakatoliki wapatao bilioni 1.4 duniani amekosoa unyonyaji kwenye bara hilo unaofanywa na mataifa ya kigeni na mashirika ya kimataifa.

Alipowasili hii leo Jumatatu kwenye jiji la Saurimo, Papa Leo XIV alitembelea makao ya wazee katika jiji hilo la mashariki mwa Angola, kuwasalimia wazee, na kuwapa zawadi. Akizungumza kwa Kireno, Papa Leo ameisifu hatua hiyo ya kuwalea wazee walio katika mazingira magumu kwa kusema hakika hiyo ni ishara muhimu sana na kipimo cha ubora wa maswala ya maisha ya kijamii ya taifa lolote lile.

Ziara ya Saurimo ilikuwa mojawapo ya mambo muhimu ya kichungaji katika safari ya Papa nchini Angola, ambayo ilianza na kuwasili kwake katika mji mkuu wa Angola Luanda mnamo Aprili 18. Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani anatarajiwa kwenda Guinea ya Ikweta hapo kesho Jumanne Aprili 21, kituo cha mwisho katika ziara yake ya siku 10 ambako atakamilisha kwa kutembelea vituo katika miji na vijiji11 kwenye nchi nne barani Afrika.

Papa Leo XIV alipotembelea makao ya wazee katika mji wa Saurimo wa mashariki mwa AngolaPicha: Vatican Media/Catholic Press Photo/IMAGO

Bara hilo ni mojawapo ya maeneo ya dunia ambako Kanisa Katoliki lina waumini wengi na wanaendelea kuongezeka. Kwa sasa kuna Wakatoliki wapatao milioni 290 wanaoishi barani Afrika. Kulingana na utabiri idadi hii ya waumini inaweza kuongezeka hadi kufikia waumini zaidi ya milioni 700 ifikapo mwisho wa karne hii. Bara la Afrika lina waumini wengi Wakatoliki kuliko wenzao wa barani Ulaya.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW