1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Leo XIV aombea amani Lebanon

1 Desemba 2025

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo XIV, Jumatatu alisali katika kaburi la mtakatifu mmoja wa Lebanon anayeenziwa mno miongoni mwa Wakristo na Waislamu nchini humo.

Papa Leo akihudhuria mkutano na viongozi tofauti wa kidini mjini Beirut
Papa Leo akihudhuria mkutano na viongozi tofauti wa kidini mjini BeirutPicha: Andreas Solaro/AFP/Getty Images

 Amefanya haya wakati alipokuwa akiwasilisha ujumbe wake wa amani, matumaini na kuvumiliana kidini katika eneo lililozongwa na machafuko.

Kengele zilisikika na maelfu ya raia wa Lebanon waliokuwa wamejipanga njiani walipiga vigelegele wakati msafara wa Papa Leo XIV ulipokuwa ukipita huko Annaya, mji ulioko karibu kilomita 40 kutoka Mji Mkuu Beirut, ukielekea katika kaburi la Mtakatifu Charbel Makhlouf.

Mbali na kupeperusha bendera za Lebanon na Vatican, baadhi walilirushia gari lililokuwa limembeba Papa maua na mchele kama ishara ya kumkaribisha.

Ujumbe wa matumaini kwa vijana

Baba Mtakatifu alisali kimya kimya ndani ya kaburi hilo lenye giza na kisha akakabidhi taa kama zawadi ya mwanga kwa nyumba ya watawa lilipo kaburi hilo. Waumini huko Lebanon wanasema Mtakatifu Makhlouf, aliwahi kufanya miujiza kadhaa ya uponyaji waumini waliposali kwa jina lake.

Papa Leo akihutubia waumini katika mkutano na maaskofu LebanonPicha: Andreas Solaro/AFP/Getty Images

Ziara ya Papa Leo katika kaburi hilo ambayo ndiyo ya kwanza kufanywa na kiongozi wa Kanisa Katoliki, ilifungua njia ya siku yake iliyokuwa na ratiba ndefu. Baada ya hapo alielekea katika mji wa Harissa ulioko kaskazini mwa Beirut, ambapo alikutana na watawa na mapadre. Aliwataka kuwapa waumini hasa vijana, matumaini katika wakati ambapo kuna uvunjifu mkubwa wa haki.

"Kama tunataka kujenga amani, ni lazima tuangalie mbinguni na tujielekeze katika njia hiyo. Tupende bila kuwa na hofu ya kupoteza vitu ambavyo vinapita na tutoe bila kipimo," alisema Papa.

Baba Mtakatifu Leo pia ataongoza kikao cha waumini wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wa dini za Kikiristo na Kiislamu katika mji Mkuu Beirut. Ni katika kikao hicho ambapo kiongozi huyo wa kidini anatarajiwa kusisitiza ujumbe wake wa amani na kuvumiliana kidini kati ya Wakristo na Waislamu nchini Lebanon na kwengineko.

Kuelekea kikao hicho, Sheikh Yahya Abdulkhalek ambaye ni kiongozi wa kidini wa kundi la wachache la Wadruze wapatikanao lebanon, Syria na Israel, amesema kikao hicho na Papa ni fursa ya kuyaleta pamoja makundi tofauti ya kidini huko Lebanon.

Machafuko na mivutano katika kiwango ambacho hakijashuhudiwa

Viongozi wa kiroho na kidini mchana wa Jumatatu walikusanyika katika uwanja mkuu wa mashahidi Beirut wakisubiri kuanza kwa kikao hicho. Miongoni mwao alikuwa Mufti Mkuu wa Wasunni Sheikh Abdel-Latif Derian na kiongozi wa Washia Sheikh Sami Abi al-Muna.

Haya yanafanyika wakati ambapo machafuko ya Gaza na mivutano ya kisiasa nchini Lebanon iko katika kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa miaka kadhaa.

papa Leo akiwasili LebanonPicha: Domenico Stinellis/AP Photo/picture alliance

Papa Leo aliwasili Lebanon Jumapili kutoka Uturuki alikokuwa ameanza ziara yake ya nje ya nchi kama Papa. Katika hotuba yake aliwataka viongozi wa kisiasa wa Lebanon kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kushirikiana ili kuwa watafuta amani wa kweli. Alitoa mwito pia kwa Wakristo nchini Lebanon kusalia nchini humo.

Wakristo nchini Lebanon ni thuluthi moja ya idadi jumla ya watu milioni 5 walioko nchini humo hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa nchi ya Kiarabu yenye idadi kubwa zaidi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati.

Vyanzo: DPA/APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW