Papa Leo XIV kufanya ziara mjini Annaba nchini Algeria
14 Aprili 2026
Kaskazini mashariki mwa Annaba, Papa Leo atatembelea mabaki ya historia ya jiji hilo, pamoja na kituo cha mapokezi kinachoendeshwa na watawa wa Kikatoliki wanaowashughulikia wazee maskini.
Wakati mmoja, mji huo ulikuwa makaazi ya Augustino, ambaye tawasifu yake ya "maungamo" ni kazi ya utafiti ndani ya utamaduni wa Kikristo.
Baadaye alasiri, Papa Leo ataadhimisha misa kwenye kanisa la mlimani la Mtakatifu Augustino mbele ya makasisi kutoka kote barani Afrika.
Papa Leo atoa wito wa msamaha
Hapo jana katika hotuba yake ya kwanza mjini Algiers, Papa Leo alitoa heshima zake kwa wahanga wa vita vya uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa Ufaransa vya 1954-1962 pamoja na kutoa wito wa "msamaha".
Pia aliwataka viongozi wa Algeria kutoogopa ushiriki mkubwa wa umma katika maisha ya kisiasa, na kutoa wito wa uhuru wa jamii ya kiraia. Papa Leo alisema mamlaka zinapaswa kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.
Tangu maandamano ya kuunga mkono demokrasia ya Hirak mnamo 2019, ambayo yalitaka mageuzi makubwa na uwazi zaidi, makundi ya haki za binadamu yameripoti kupungua kwa uhuru na kuongozeka udhibiti mkubwa wa serikali kwa wananchi.
Papa Leo anatarajiwa kuondoka Algeria kesho kuelekea Cameroon, kabla ya kusafiri kwenda Angola na Guinea ya Ikweta.
Katika hatua nyingine, kauli za hivi karibuni za Papa Leo za kutaka amani katika Mashariki ya Kati, ambako vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vimeikumba sehemu kubwa ya eneo hilo, zimeibua hasira ya viongozi wa Marekani, kwanza kutoka kwa Rais Donald Trump na sasa makamu wake, JD Vance.
JD Vance aungana na bosi wake kumshtumu Papa Leo
Hapo jana wakati wa mahojiano na shirika la habari la Fox News, Vance aliulizwa maoni yake kuhusu shutuma za Rais Trump dhidi ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, ambapo alisema kuwa katika baadhi ya matukio, ni vyema kwa Vatican kuzingatia tu masuala ya maadili:
''Vatican inapaswa kuzingatia masuala ya kinachoendelea katika Kanisa Katoliki na kumwacha rais wa Marekani kusimamia sera za umma za Marekani. Lakini wanapokuwa kwenye mzozo, ndio wako kwenye mzozo. Sijali sana kuhusu hilo, lakini nadhani ni jambo la kawaida. Nina hakika itatokea katika siku zijazo, na sio suala kubwa kama lilifanyika awali.''
Kupitia mtandao wake wa Truth Social hapo jana Rais Trump alimtaja Papa Leo kuwa mtu dhaifu dhidi ya uhalifu na asiyefaa kuzungumzia sera ya kigeni ya nchi yake.