1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Mstaafu Benedict wa 16 aaga dunia akiwa na miaka 95

John Juma Mhariri: Zainab Aziz
31 Desemba 2022

Kiongozi wa zamani wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa mstaafu Benedict wa 16 ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 95.

Papst Benedikt
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Vatican, makao makuu ya kanisa Katoliki imetangaza tanzia hiyo ya Benedict na kusema alifariki Jumamosi asubuhi. Benedict ambaye majina yake kamili ni Joseph Ratzinger alikuwa papa wa kwanza Mjerumani baada ya kipindi cha takriban miaka 500.

"Kwa majonzi makubwa, ni lazima nitangaze kwamba Benedict wa kumi na sita, papa wa zamani, aliaga dunia saa 9:34 leo asubuhi kwenye Monasteri ya Vatican, ambako amekuwa akiishi tangu alipostaafu mwaka 2013,” ametangaza msemaji wa Vatican Matteo Bruni.

Hali ya wasiwasi kuhusu afya ya Benedict ilianza Jumatano pale Papa Francis alitangaza kuwa afya yake imedhoofika sana na kutaka watu wamuombee. Papa Francis pia alimtembelea huyo mtangulizi wake katika makazi yake.

Vatican haijakuwa ikitoa maelezo kamili kuhusu ugonjwa wa Benedict. Badala yake imekuwa ikisema tu kuwa hali yake imezidi kudhoofika kutokana na umri wake.

Papa Francis amtembelea papa mstaafu Benedict anayeumwa

Papa wa kwanza kujiuzulu baada ya karne nyingi

Benedict aliwashangaza wengi alipotangaza kujiuzulu mnamo Februari 28, 2013. Alikuwa papa wa kwanza kuwahi kuchukua hatua kama hiyo ya kustaafu katika karne nyingi, akitoa sababu ya umri wake na hali yake ya afya.

Papa mstaafu Benedict XVI (kulia) akiwa na mrithi wake Papa Francis mjini Vatican Juni 28, 2017.Picha: L'Osservatore Romano/Pool Photo/AP/picture alliance

Hatua yake ilimsafishia njia mrithi wake kutoka Argentina Papa Francis. Tangu wakati huo, papa mstaafu Benedict amekuwa akiishi kwa faragha katika nyumba ya watawa huko Vatican.

Waumini wamuaga Papa

Mwili wake utapelekwa katika mazingira matakatifu ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, kuanzia Jumatatu asubuhi ili kuruhusu waumini kutoa heshima zao za mwisho.

Mazishi ya Benedikt wa 16 yataongozwa na kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis kwenye kanisa kuu la mtakatifu Petro tarehe 5 Januari.

Viongozi watuma risala za rambirambi

Viongozi duniani kote wametoa salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Benedict. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema dunia imempoteza mwanathiolojia aliyekuwa na ushawishi mkubwa.

Kansela Scholz ameeleza kuwa Benedict wa 16 alikuwa kiongozi mahsusi wa kanisa siyo nchini Ujerumani tu.

Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni amesema Benedikt wa 16 alikuwa nguzo ya imani na busara na kwamba dunia itaendelea kumkumbuka.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema Wakatoliki wote wamempoteza kiongozi aliyefanya kazi kwa moyo wake wote na kwa busara kwa ajili kujenga dunia ya undugu.

Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen pia ametoa rambirambi kwa niaba ya Umoja wa Ulaya kufuatia kifo cha aliyekuwa Papa Benedict wa 16 leo Jumamosi.

Waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amesema amesikitishwa juu ya kifo cha baba mtakatifu wa zamani Ratzinger aliyewahi kufanya ziara ya kihistoria nchini Uingereza mnamo mwaka 2010. 

Papa Benedict XVI alitajwa kuwa mwanatheolojia mahiri, lakini uongozi wake ulikumbwa na kashfa za manyanyaso ya kingono dhidi ya watoto.Picha: Domenico Stinellis/AP Photo/picture alliance

Mnamo mwaka 2005, watu waliruhusiwa kuutizama mwili wa aliyekuwa mtangulizi wa Benedict John Paul II, ambaye ndiye alikuwa papa wa mwisho kuaga dunia. Mwili huo uliwekwa katika katika viwanja vya Vatican na watu milioni moja wakiwemo wakuu wa nchi walitoa heshima za mwisho.

Kashfa za dhuluma za ngono dhidi ya watoto

Benedict alitajwa kuwa mwanatheolojia mahiri. Lakini upapa wake ulikumbwa na mivutano ya ndani kwa ndani mjini Vatican na vilevile kashfa za makasisi kuwanyanyasa watoto kingono, matukio yaliyolitikisa kanisa la Katoliki ulimwenguni kote, na alikosolewa kwa kukosa kuonyesha uongozikuhusu hilo.

Dhuluma hizo za ngono ziligubika miezi ya mwisho wa uhai wake, baada ya ripoti ya kanisa la Ujerumani ya Januari 2022, kumshutumu moja kwa moja kwa kushindwa kuwazuia makasisi wanne waliokuwa wakiwadhulumu watoto kingono miaka ya 1980 alipokuwa askofu mkuu wa Munich.

Aliyakana madai dhidi yake na Vatican ilitetea vikali rekodi yake ya kuwa papa wa kwanza kuomba radhi na kuelezea masikitiko yake makubwa kutokana na kashfa hizo na vilevile alikutana na wahanga wa kadhia hizo.

Alizaliwa Aprili 16, 1927 katika eneo la Marktl am Inn, jimbo la Bavaria nchini Ujerumani.

Aliteuliwa kuwa papa alipokuwa na umri wa miaka 78.

Vyanzo: DPAE, AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW