Papa: Waliofunga ndoa hawatakuwa mapadri
12 Februari 2020Huu ungekuwa uamuzi wa kipekee katika sheria ya muda mrefu ya mapadri kutofunga ndoa.
Uamuzi huo ambao ingawa ungekuwa ni wa eneo la Amazon pekee, ungewaghadhabisha wahafidhina ambao tayari wanauchukulia uongozi wa Papa Francis kama wenye misimamo mingi ya wastani.
Miongoni mwa wahafidhina hao ni kama Kadinali Robert Sarah ambaye mwezi uliopita alichapisha kitabu kilichotetea hatua ya mapadri wa Kanisa Katoliki kutofunga ndoa. Papa mstaafu Benedict wa Kumi na Sita pia alihusika katika uandishi wa kitabu wa hicho.
Watu ambao si mapadri hawatatoa sakramenti muhimu
Katika waraka uliosubiriwa kwa hamu, Papa hata hakuzungumzia chochote kuhusiana na mapendekezo ya maaskofu wa Amazon kuhusiana na suala la kuwafikiria wanaume walio kwenye ndoa kuwa mapadri na wanawake kuwa mashemasi.
Vile vile ameondoa uwezekano wa watu ambao si mapadri kutoa sakramenti muhimu za kupokea na kitubio. Badala yake amewataka maaskofu waombee miito ya kipadri na wawatume wamishonari katika eneo hilo ambapo waumini Wakatoliki wanaweza kwenda miezi au hata miaka bila kufanyiwa misa.
Kiongozi huyo wa dini amewashusha mabega wale waumini walio na usasa ambao walikuwa wanatarajia kwamba angaliweka suala hilo kwa mazingatio ya baadaye.
Katika mkutano wa kilele wa mwezi Oktoba uliojulikana kama Synod, maaskofu wa Amazon walitoa wito wa wanaume walio katika ndoa kukubaliwa katika upadri katika eneo lao tu ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa mapadri ulioko katika eneo hilo.
Papa ameyapa jina "Mpendwa Amazon" mawasiliano yake
Uhaba huu wa mapadri umewapelekea Wakristo Wakatoliki katika eneo la Amazon kuvutiwa na kujiunga na makanisa ya Protestant na Pentekosti ambapo waumini wanashirikishwa misa za mara kwa mara.
Papa ameyaweka rasmi maoni yake katika mawasiliano aliyoyaita "Mpendwa Amazon" ambayo ni kama barua ya mapenzi kwa msitu wa Amazon na watu wanaoishi katika eneo hilo. Kwa muda mrefu Papa Francis amekuwa na wasiwasi kuhusiana na uharibifu wa msitu huo, umuhimu wake katika mazingira na ukiukaji wa haki ambao umekuwa ukifanyiwa watu wanaoishi katika msitu huo.
Papa amesema analiombea eneo la Amazon na anatarajia kwamba haki za maskini pamoja na utajiri wao wa kitamaduni utaheshimiwa, uzuri wa kiasili wa msitu huo utahifadhiwa na Wakristo wa eneo hilo waonyeshe ishara zao.