Paraguay yatamba na Italia mambo bado magumu
20 Juni 2010New Zealand imetoka sare ya bao 1-1 na Italia na kuvuruga nafasi za mabingwa hao watetezi wa Kombe la Dunia kuongoza katika kundi lao la F.
Mbele ya watazamaji 38,000 katika uwanja wa Mbombela huko Nelspruit watoto wa New Zealand waliweza kuufuma wavu wa Italia na mapema kutokana na bao la Shane Smeltz alietumia fursa ya kosa la ulinzi la nahodha alie na umri mkubwa Fabio Cannavaro.Italia ilijazana mbele lakini,iliishia kusawazisha tu kwa kupitia mkwaju mzuri wa penelti uliopigwa na Vincenzo Laquinta katika dakika ya 29.
Licha ya kuiisakama lango la New Zealand na wachezaji watatu wa kushambulia Italia imethibitisha maneno ya wale wanaoamini kuwa washambuliaji wengi haimaanishi kufunga magoli mengi.
Matokeo hayo yameiacha Italia kuwa na pointi mbili tu na Paraguay inaongoza kundi lao kwa kuwa na pointi nne baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Slovakia mechi ya kwanza ya Jumapili.Nafasi ya Italia kuongoza kundi lao sasa ni finyu sana.
Italia katika mechi ya ke ya mwisho inakumbana na Slovakia wakati New Zealand itacheza na vikaka Paraguay
Paraguay imeiangusha Slovakia katika mechi ya awali na kuendeleza kutamba kwa Amerika ya Kusini katika michuano ya kuwania Kombe la Dunia inayoendelea nchini Afrika Kusini.
Huko Bloemfontein timu kakamavu ya Paraguay imetoka kifua mbele uwanjani baada ya kuwabwaga Slovakia mabao 2-0 ambayo yaliwekwa wavuni na Enrique Vera na mkwaju wa dakika za mwisho uliochomekwa na Cristian Riveros na kuwaacha katika nafasi nzuri ya kuweza kusonga mbele katika duru ya pili ya michuano hiyo.
Timu za Amerika ya Kusini zimen'gara katika michuano ya mwanzo ya Kombe la Dunia kwa kujipatia ushindi wa mechi saba,kutoka sara mara tatu na kufungana wenyewe kwa wenyewe katika mechi moja tu ambapo Chile iliifunga Honduras.
Katika mpambano wa kukata na shoka wa Jumapili usiku kocha wa Brazil Dunga atakabiliana na kocha wake zamani Sven-Goran Eriksson ambaye sasa ni kocha wa Ivory Coast katika mpambno wa kundi G huko Soka City mjini Johannesburg.
Chini ya Dunga Brazil ilibadili mtindo wake mashuhuri wa soka wa samba iliokuwa ikicheza na badala yake kucheza kwa nidhamu zaidi kwa kupunguza mbwembwe uwanjani hatua ambayo imewapotezea baadhi ya mashabiki. Eriksson hakuwa na la kusema isipokuwa kumwagia sifa Dunga ambaye alimfundisha alipokuwa na umri wa miaka 25 katika timu ya Florentina hapo mwaka 1988 -1989.Msweden huyo amekaririwa akisema kwamba Dunga ni mmojawapo wa wasakata dimba wazuri kabisa kuwahi kuwa nao na ndio maana hashangazwi na jinsi timu yake ilivyoandaliwa vyema sana.
Kuongezea chapuo katika mpambano huo, mshambuliaji wa Ivory Coast Didier Drogba atapambana upya na mlinzi wa Brazil Lucio baada ya kukumbana katika mechi kali wakati Chelsea ilipokwaruzana na Inter Milan katika ligi ya mabingwa.
Mwandishi Mohamed Dahman/ RTRE/AFP
Mpitiaji :P.Martin