1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PARIS: Lebanon yapata misaada ya kifedha katika kikao cha wafadhili, Ufaransa.

25 Januari 2007

Saudi Arabia imeahidi itaipatia Lebanon msaada wa karibu Euro mia nane.

Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Saudi al-Faisal ametangaza msaada huo mjini Paris, Ufaransa kwenye kikao cha wafadhili kinacholenga kusaidia kukarabati Lebanon iliyoharibiwa kwa kiasi kikubwa wakati wa vita vya mwaka uliopita kati ya Israil na wanamgambo wa Hizbullah.

Rais wa Ufaransa, Jacque Chirac; pia ameahidi Ufaransa itaipa serikali ya Fuad Siniora mkopo wa Euro mia tano.

Umoja wa Ulaya tayari umeahidi kutoa msaada wa Euro milioni mia nne kwa miaka mitano ijayo.

Waziri Mkuu wa Lebanon, Fuoad Siniora, amekiarifu kikao hicho serikali yake itajaribu kusuluhisha kwa njia ya amani mzozo kati yake na upande wa upinzani unaoongozwa na chama cha Hizbullah.

Waziri Mkuu huyo alisema:

"Tutaendelea kushirikiana na wenzetu wa upande wa upinzani kupata suluhisho la kidemokrasia kwa matatizo yetu. Raia wa Lebanon wana uzoefu wa kukabiliana na matatizo yao. Mashauriano ya amani ndio njia ya pekee ya kutanzua tofauti zetu za kisiasa"

Kikao hicho kimeandaliwa siku mbili baada ya watu watatu kuuawa na wengine kadha wakajeruhiwa nchini Lebanon kwenye mgomo mkubwa ulioitishwa na chama cha Hizbullah ambacho kinataka kuiangusha serikali.

Wakati huo huo, kiasi mwanafunzi mmoja wa upinzani ameuawa kwa kupigwa risasi kwenye mapambano kati ya makundi ya wanafunzi yanayopingana katika Chuo Kikuu cha Beirut:

Walioshuhudia wamesema makundi hayo ni ya wanafunzi wanaounga mkono upinzani na wale wanaounga mkono serikali.

Haijaeleweka waziwazi aliyempiga risasi mwanafunzi huyo kichwani mwake.

Kituo cha televisheni cha Al-Manaar kinachosimamiwa na chama cha Hizbullah kimedai mwanafunzi huyo ameuawa na wanamgambo wanaounga mkono serikali na ambao ni wafuasi wa kiongozi wa Wasunni, Saad al-Hariri.

Kiasi watu ishirini na watano wamejeruhiwa kwenye mapambano hayo.