1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PARIS: Machafuko yapungua mjini Paris, Ufaransa

9 Novemba 2005

Machafuko yaliendelea usiku wa kuamkia leo mjini Paris, Ufaransa, lakini hatua ya serikali kutaka kutangaza misako inaonekana imeanza kufaulu katika kuyazima machafuko hayo, ambayo yamekuwa yakiendelea kwa karibu majuma mawili.

Waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo Nicolas Sarkozy, amesema polisi wamethibitisha kupungua kwa machafuko katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Serikali ya Ufaransa ilitangaza hali ya hatari katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na machafuko hayo, hatua itakayowaruhusu maofisa katika maeneo hayo kutangaza misako ya usiku kucha kukabiliana na ghasia ambazo zimeelezwa kuwa mbaya zaidi tangu machafuko ya wanafunzi ya mwaka wa 1968. Amri hiyo ilichapishwa rasmi hapo jana na itaanza kutekelezwa hii leo.

Mji wa kazkazini wa Amiens ulikuwa wa kwanza kutangaza msako kwa watu wote chini ya miaka 16 na kupiga marufuku kuuziwa mafuta ya petroli vijana wadogo.