1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PARIS : Sarkozy na Royal katika marudio ya uchaguzi wa rais

23 Aprili 2007

Kiongozi wa kihafidhina Nicolas Sarkozy ameongoza vizuri katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais nchini Ufaransa hapo jana na atapambana na mpizani wake wa Kisoshalisti Segolene Royal katika marudio ya uchaguzi huo hapo tarehe 6 mwezi wa Mei.

Sarkozy waziri wa zamani wa mambo ya ndani ameahidi kuwafaidisha watu wanaofanya kazi kwa bidii na kupiga vita uhalifu na anaonekana yuko katika nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi huu baada ya kujinyakulia idadi kubwa ya kura kuwahi kuzolewa na mgombea wa urais wa sera za mrengo wa kulia tokea mwaka 1969.

Wakati takriban kura zote zikiwa zimehesabiwa Sarkozy amejizolea asilimia 31 ya kura wakati Royal amejipatia asilimia 24 na ushee.Christian Bayrou mgombea wa sera za wastani ameshika nafasi ya tatu kwa kujipatia asilimia 18 na ushee na kiongozi wa sera kali za mrengo wa kulia Jean- Marie le Pen ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa rais mwaka 2002 ameshika nafasi ya nne kwa kujipatia asilimia 11 ambayo ni ndogo kabisa kuwahi kujipatia katika majaribio yake matatu yaliopita ya kuwania urais.

Asilimia 85 ya watu waliojitokeza kupiga kura ni kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 50 nchini Ufaransa.

Uchaguzi huo unatafuta mrithi wa Rais Jaques Chirac ambaye anan’gatuka baada ya kuwa madarakani kwa miaka 12.