Paris: Ushahidi wa magereza ya CIA barani Ulaya.
9 Juni 2007Mchunguzi mmoja wa bara la Ulaya amesema ana ushahidi kwamba Poland na Romania zilikuwa na magereza ya siri ya shirika la ujasusi la Marekani, CIA, kwa misingi ya mwafaka uliyowekwa wa kuwasaka na kuwahoji washukiwa wa ugaidi waliokuwa wakitafutwa na Marekani.
Seneta wa Uswisi, Dick Marty, amesema Poland iliwashikilia baadhi ya washukiwa wakuu wa CIA, akiwemo Khalid Sheikh Mohammed, anayedai kwamba ndiye aliyepanga mashambulio ya tarehe kumi na moja Septemba mwaka 2001 nchini Marekani.
Dick Marty amesema kwenye taarifa ya kitengo cha kutetea haki za binadamu barani Ulaya kwamba habari za uhakika zipo zinazothibitisha kwamba kutoka mwaka 2003 hadi mwaka 2005 kulikuwa na magereza ya CIA barani Ulaya.
Makamu rais wa kundi la wabunge wa Umoja wa Ulaya, Erik Jürgens amesisitiza kwamba ushahidi huo ni mzito
Erik Jürgens anasema anaamini ushahidi upo wa kutosha hasa orodha ya ndege zilizowasili zikielekea hususan nchini Poland ingawa serikali imekuwa ikikanusha kuwepo kwa safari hizo za ndege.
Kiongozi huyo amesema wana ushahidi mzito unaoonyesha kwamba ndege hizo zilitua nchini Poland na hatua ya serikali kukanusha inathibitisha kwamba ndege hizo hazikwenda huko kwa nia safi.
Seneta Dick Marty amemlaumu rais wa zamani wa Poland, na pia rais wa sasa na marais wa zamani wa Romania kwamba walijua na wakaidhinisha harakati za CIA nchini mwao.
Poland na Romania, ambazo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya, mara kwa mara zimekuwa zikikanusha habari kwamba zilikuwa na magereza ya siri.