1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Paris yaanza kuwaondoa wahamiaji

7 Novemba 2019

Polisi nchini Ufaransa imewaondoa wahamiaji waliokuwa kwenye makambi mawili makubwa kabisa kaskazini mwa mji mkuu Paris hii leo huku mamlaka za nchi hiyo zikiapa kuwaondoa wahamiaji kwenye makambi mengine yaliyosalia.

Frankreich, Paris: Obdachlose Immigranten schlafen auf der Straße
Picha: picture-alliance/AP/F. Mori

Wahamiaji 1,600 waliokuwa wakiishi kinyume cha utaratibu kwenye mahema yaliyokuwa maeneo ya Porte de la Chapelle na Seine-Saint Denis wamechukuliwa hii leo na mabasi.

Mkuu wa jeshi la polisi jijini Paris Didier Lallement amewaambia waandishi wa habari kwamba hataendelea kuvumilia ujenzi wa mahema pembezoni mwa barabara ama mahala pengine popote pa wazi kwenye jiji hilo.

Wahamiaji hao ambao wengi wao ni wanaume wanaotoka mataifa ya kusini mwa Sahara na baadhi kutoka Mashariki ya Kati waliingia kwenye mabasi hayo na kupelekwa kwenye majumba ya mazoezi ya viungo ama gym na wengine wakipelekwa kwenye viwanja vilivyopo Paris. Wakati huohuo mashine za kuchimbua zikivunja mahema hayo kubeba viti vya plastiki, magodoro na matakataka, mahala ambako waliishi wahamiaji hayo.

Mmoja wa wahamiaji walioondolewa Muhamad Rafeh aliyotokea Afghanistan alilalama kwamba mazingira kwenye eneo hilo yalikuwa ni mabaya mno na hayakuwa ya kiutu. Alisema "Hali ni mbaya sana kwa wahamiaji wote wa hapa. Siyo mazingira mazuri. Kuna baridi kali, hali ya hewa ni ya baridi sana. Lakini pia, kila wakati kuna mvua, ardhi huwa mbichi. Hapafai kwa kuishi hapa."

Polisi imesema itaendelea kuwepo mahala hapo wakati wote katika kipindi cha wiki kadhaa zijazo ili kuwazuia wahamiaji hao kurejea.

Kambi kubwa ya Calais ilipofungwa mwaka 2016, wahamiaji wengi walikimbilia jijini Paris.Picha: picture-alliance/dpa/La Voix Du Nord/M. Demeure

Waziri mkuu wa Ufaransa Eduardo Philippe hapo jana alitangaza kufungwa kwa makambi ya mahema, viwango vya wahamiaji wanaofanya kazi pamoja na ukomo katika upatikanaji wa huduma za afya zisizo za dharura kwa waomba hifadhi wapya hii ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kukabiliana na hofu ya wapiga kura kuhusiana na wahamiaji.

Tangu kufungwa kwa kambi kubwa kabisa ya Calais mnamo mwaka 2016 wakimbizi wengi wakahamia Paris ambako mara kadhaa walivunjiwa makambi ingawa walirejea tena lakini kwenye maeneo mengine miezi michache baadae.

Meya wa Paris Anne Hildago amesema ingawa viongozi wa jiji hilo walimueleza mara kwa mara kwamba makambi hayo hayatarejea tena lakini tofauti na hivyo, yalirudi. 

Naibu meya Emmanuel Gregoire alisema, mbali na kambi ya Porte de la Chapelle kulikuwa na wahamiaji wengine 1,600 kwenye kambi jirani ya Porte d'Aubervilliers na makambi mengine yaliyopo Porte de la Villete na Seine-Saint Denis yote yakiwa kaskazini mwa Paris.

Waziri wa mambo ya ndani Christophe Castaner amesema, watu waliohamishwa hii leo watapewa makaazi kwenye vituo vinavoyendeshwa na serikali, wakati maombi yao ya hifadhi yakiendelea kushughulikiwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW