PARIS:Ufaransa kuongoza jeshi la kimataifa la kulinda amani Lebanon
17 Agosti 2006Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa bibi Michele Alliot Marie amesema nchi yake imekubali kuliongoza jeshi la kimataifa la kulinda amani kusini mwa Lebanon, lakini amesema jukumu la jeshi hilo lazima kwanza lifahamike wazi.
Bibi Michele Alliot Marie pia ametaka jeshi hilo liwe na nguvu za kutosha.
Utayarifu wa Ufaransa kuliongoza jeshi hilo unafuatia juhudi zinazofanywa kwenye Umoja wa Mataifa na nchini Lebanon kwa lengo la kupata askari alfu tatu na mia tano wa kwanza watakaowekwa kusini mwa Lebanon baada ya majeshi ya Israel na wapiganaji wa Hezbollah kukubali kuacha mapigano.
Lengo la Umoja wa Mataifa ni kupeleka jeshi la askari alfu 15, kwa mujibu wa azimio lililopitishwa ijumaa iliyopita.
Wakati huo huo askari alfu 15 wa Lebanon leo wanatarajiwa kuanza kulinda sehemu muhimu za kusini mwa nchi hiyo.
Askari hao pamoja na wa jeshi la kimataifa watasimamia sehemu zilizokuwa chini ya udhibiti wa wapiganaji wa Hezbollah,
Na Israel imeendelea kuondoa askari wake kutoka kusini mwa Lebanon na kukabidhi udhibiti wa sehemu hiyo kwa askari wa jeshi la Umoja wa Mataifa.