1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pasaka yaadhimishwa Ukraine ikizidi kushambuliwa

17 Aprili 2022

Mamilioni ya Wakristo wanasherehekea sikukuu ya Pasaka kukumbuka kufufuka kwa Yesu Kristo baada ya kusulubiwa msalabani zaidi ya miaka 2000 iliyopita, huku mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine yakiendelea kupamba moto.

Messfeier zur Osternacht im Petersdom
Picha: Tiziana Fabi/AFP

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, ameutumia ujumbe wake wakati wa misa ya Mkesha wa Pasaka kulaani kile alichokiita ukatili wa vita unaoshuhudiwa nchini Ukraine.

Bila kuitaja moja kwa moja Urusi, Baba Mtakatifu ametoa wito wa kuwepo usitishaji mapigano katika siku ya Pasaka kwa malengo ya kufikia makubaliano ya amani kwa njia ya mazungumzo.

Hayo yanajiri wakati jeshi la Urusi likivitolea mwito vikosi vya Ukraine katika mji wa bandari uliozingirwa wa Mariupol kuweka chini silaha na kujisalimisha likionya kwamba kutakuwa na "taathira kubwa" baada ya muda uliowekwa kumalizika.

Muda wa mwisho kwa Mariupol 

Raia wakipita mbele ya vifaru vya Urusi katika mji wa Mariupol siku ya tarehe 15 Aprili 2022.Picha: Sergei Bobylev(TASS/picture alliance

"Kwa kutilia maanani janga baya linaloendelea kwende kiwanda cha chuma cha Azovstal, na pia kwa kuongozwa na misingi ya kibinaadamu, Jeshi la Urusi linawapa wapiganaji wa vikosi vya siasa kali za kizalendo na mamluki wa kigeni muda kuanzia saa 12:00 asubuhi (kwa majira ya Moscow) ya tarehe 17 Aprili 2022, kuacha mapigano na kuweka silaha zao chini", ilisema wizara ya ulinzi ya Urusi kwenye taarifa yake.

"Wote ambao wataweka silaha zao chini wanahakikishiwa usalama wa maisha yao," ilisema ripoti hiyo, ikiongeza kwamba wapiganaji hao wanapaswa wamwe wameshaondoka kwenye kiwanda hicho ifikapo saa 4:00 asubuhi wakiwa hawana silaha yoyote.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema vikosi vyake vilishalisafisha eneo lote la mjini Mariupolna kwamba ni kikosi kidogo tu cha wapiganaji waliosalia ndani ya kiwanda cha chuma cha chuma kufikia siku ya Jumamosi (Aprili 16).

Hakukuwa na jibu la haraka kutoka Kyiv, ingawa Rais Volodymyr Zelenskyy aliliambia shirika la habari la Ukrainska Pravda kwamba hali ni mbaya sana. 

Zelenskyy akiri hali kuwa ngumu

Rais Volodymyr Zelenskyy akizungumza kwa njia ya video kwenye hotuba zake za kila siku kwa taifa.Picha: Ukrainian Presidential Press Office/AP/dpa/picture alliance

"Wanajeshi wetu wamezingirwa, majeruhi wamezingirwa. Kuna hali mbaya ya kibinaadamu... Licha ya hayo, vijana wetu wanajilinda." Alisema kiongozi huyo.

Maelezo yaZelenskyyyanalingana na yale ya Urusi kwamba wapiganaji wote wa mwisho wa Ukraine katika mji wa Mariupol wamezingirwa katika majengo ya kiwanda cha kufua chuma cha Azovstal.

Zelenskyy alisema amezungumza kwa njia ya simu na viongozi wa Uingereza na Sweden kuhusu hali kwenye mji wa Mariupol anayosema kuwa ya hatari na kwamba Urusi inajaribu kumuangamiza kila mtu kwenye eneo hilo.

Madai ya Moscow kwamba ilishachukuwa udhibiti kamili wa mji wa Mairupol, eneo ambalo limeshuhudia mapigano makali na hali mbaya kabisa ya kibinaadamu, hazikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru.

Endapo Mariupol itatekwa, utakuwa mji wa kwanza kuangukia mikononi mwa vikosi vya Urusi tangu ianzishe uvamizi wake Februari 24.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW