1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Paul Kagame-Kiongozi mwenye maono, dikteta au vyote?

Sekione Kitojo
1 Agosti 2017

Rais wa Rwanda Paul Kagame, aliyeko madarakani kwa miaka 17, ametabiri kwamba atashinda uchaguzi wa Agosti 4 kwa wingi mkubwa akiungwa mkono kutawala kwa muhula wa tatu, akipuuzia shutuma za kuzuwia mijadala ya kisiasa.

Paul Kagame
Picha: Picture alliance/AP Photo/E. Murinzi

Paul Kagame  anatukuzwa  kwa  kusitisha  mauaji  ya  kimbari  nchini Rwanda na  kuielekeza  nchi  hiyo  katika  kile wale  wanaomsifu wanakiita  maajabu ya  kiuchumi, lakini  wakosoaji  wake wanamuona kama  dikteta , mtawala  mwenye  mamlaka yote  ambaye anaukandamiza  upinzani na  anatawala  kwa  kuleta  hofu.

Rais Paul Kagame akiwa katika moja ya mikutano yake ya kampeni nchini RwandaPicha: Picture alliance/Zumapress/G. Dusabe

Kiongozi  huyo mwenye umri  wa  miaka  59 mpiganaji  wa  zamani wa  chini  kwa  chini  anawania  muhula  wa  tatu madarakani  katika uchaguzi  wa  hapo  Ijumaa  Agosti 4 baada  ya  wapiga  kura kuidhinisha  kwa  wingi mabadiliko  ya  katiba  ili  Kagame  agombea tena  na  kubakia  madarakani  kwa  miongo  mingine miwili.

Kagame  anasema  hatua  yake  ya  kuwania  madaraka  ni wajibu kwa  nchi  yake, hata  hivyo  hatua  hiyo  imewakasirisha  washirika wa  kimataifa  ambao uvumilivu  wao  unavikia  mwisho kwa  mtu huyo  ambaye  alikuwa  akionekana  kama  mfano wa  mafanikio katika  uongozi  wa  bara  la  Afrika  baada  ya  kipindi  cha  ukoloni.

Hata  hivyo  rais  wa  nchi  hiyo  ndogo ya  Afrika  ya  kati  amekuwa mmoja  katika  viongozi  wenye  nguvu  kabisa  katika  bara  la  Afrika na  wanaosifiwa  sana. Wenzake , wanatiwa  hamasa  na mabadiliko  nchini  Rwanda , wamempa  jukumu  la  kubadilisha Umoja  wa  Afrika.

Rais Paul Kagame akiwa katika mkutano wa viongozi wa Afrika mjini Addis AbabaPicha: picture-alliance/abaca/M. Wondimu Hailu

Mauaji  ya  kimbari

Nchi  hiyo  iliyovurugika  kutokana  na  mauaji  ya  kimbari ya  mwaka 1994  na  bila  ya  kukuta  kipande  cha  ndururu  ya  fedha   katika hazina  ya  taifa Kagame  aliingia  madarakani, na  Rwanda  hivi sasa  inaukuaji  wa  uchumi  unaofikia  kwa  wastani  wa  asilimia  7 kwa  mwaka   wakati  mji  mkuu  Kigali  umebadilika  na  kuwa  mji mkuu  wenye  majengo  mazuri, safi, mitaa  salama  na  kutokuvumilia kabisa  rushwa.

"Kagame  anafahamika  kuwa  ni  mchapa kazi  na  mtekelezaji, na sio  mtu ambaye  anasema  mambo  tu  kama  watu  wengine," amesema  Desire Assogbavi , mratibu  wa  shirika  la  Oxfam  katika Umoja  wa  Afrika  ambaye  anaandika  mara  kwa  mara  katika blogu  yake kuhusu  taasisi  hiyo ya  Afrika.

Rafiki  wake  wa  karibu  Tony Blair anamsifu kuwa  ni  "kiongozi mwenye  maono" kutokana  na  maendeleo  makubwa  aliyoiletea nchi  yake.

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony BlairPicha: picture alliance/empics/J. Brady

Wajihi  wa  rais  huyo , unaoelezwa  kuwa "dikteta asiye  na msamaha"  na  mwandishi Philip Gourevitch , ambaye  aliandika maenezo mazito  juu  ya  mauaji  ya  kimbari, ulitengenezeka  wakati akikua  uhamishoni.

Uhamishoni

Mwaka  1960, wakati  akiwa  na  umri  wa  miaka  mitatu , familia yake  ya jamii  yenye uwezo  ya  Watutsi  ilikimbilia  katika  nchi jirani  ya  Uganda ikikimbia mauaji  ya  halaiki nchini  mwao.

Akitumikia  jeshi  la  waasi  waliokuwa  wakiongozwa  na  rais Yoweri Museveni  kabla  na  baada  ya  kukamata  madaraka  mwaka 1986, alipanda na  kuwa  mkuu  wa  kitengo  cha  usalama  wa  taifa.

Rais wa zamani wa Rwanda Juvenal HabyarimanaPicha: picture-alliance/dpa

Kagame ambaye  ni  rais  pekee  anafahamika  kupata  mafunzo  ya kijeshi nchini  Marekani  na  Cuba, baadaye  alichukua  uongozi wa kikundi  kidogo  cha  waasi  wa  Rwanda  wanaoishi  uhamishoni ambao  walijipenyeza  ndani  ya  Rwanda  wakitarajia  kuiangusha serikali ya  rais Juvenal Habyarimana mwaka  1990, na  kuzusha vita  vya  wenyewe  kwa  wenyewe.

Pamoja na jeshi lililoangushwa kutoka madarakani, wakimbizi wengi waliingia katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutoka RwandaPicha: picture-alliance/dpa

Kifo  cha  Habyarimana  katika  ajali  ya  ndege  kilizusha  miezi mitatu  ya  mauaji  ya  kimbari  mwaka  1994, wengi  wao  wakiwa Watutsi  waliouwawa  na  vijana  wa  Kihutu  ambao  ni  kabila  lenye watu  wengi  nchini  humo  wakihimizwa  na  kauli  za  chuki.

Kagame baba  wa  watoto  wanne, alikuwa  na  umri  wa  miaka 36  wakati huo  jeshi  la  wasi  wa  Rwandan Patriotic Front  RPF lilipoyafurusha majeshi ya  Rwanda  ambayo  yaliwauwa  watu  wanaokadiriwa kufikia  800,000 na  kuukamata  mji  mkuu  Kigali, na  kuwa  kiongozi rasmi  wa  nchi  hiyo.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW