1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Paul Kagame kusalia madarakani hadi mwaka 2034?

Angela Mdungu
15 Julai 2024

Rwanda inafanya uchaguzi mkuu leo Julai 15, 2024. Rais Paul Kagame ambaye anatarajiwa bila shaka kupata ushindi wa kishindo katika azma yake ya kuwania muhula wa nne madarakani.

Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwa kwenye kampeni ya uchaguzi
Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwa kwenye kampeni ya uchaguziPicha: Jean Bizimana/REUTERS

Paul Kagame ni kiongozi maarufu nchini Rwanda ambaye baadhi ya watu wanamchukulia kama shujaa aliyeweza kuyazima mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 na pia kuwa na maono ya kurejesha amani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Lakini baadhi ya watu wanamchukulia Kagame kama kiongozi dhalimu, mwenye msimamo mkali na anayetawala kwa misingi ya hofu na ukandamizaji.

Kagame aliyepata mafunzo ya kijeshi nchini Marekani na Cuba na kutoka kabila la watutsi, alikimbilia nchini Uganda na familia yake mwanzoni mwa miaka ya 1960 ili kuepuka mauaji ya kimbari. Alishirikiana na rais wa sasa wa Uganda Yoweri Museni wakati wa harakati zake za kuchukua mamlaka na aliteuliwa kuwa mkuu wa idara ya ujasusi wa nchi hiyo kabla ya kuanzisha mnamo miaka ya 1990, vuguvugu la kuupindua utawala wa Wahutu uliokuwa ukiongozwa na Juvenal Habyarimana.

Soma pia: HRW yaishutumu Rwanda kwa mauaji ya wakosoaji nje ya nchi

Alikuwa na umri wa miaka 36 tu wakati kikosi chake cha waasi cha Rwandan Patriotic Front (RPF) kilipowashinda Wahutu wenye itikadi kali wa "Interahamwe" ambao kwa muda wa siku 100, walikuwa wamewaua mamia ya maelfu ya Watutsi wakati wa mauaji hayo ya kimbari ya mwaka 1994. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu 800,000 waliuawa.

Wagombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2024 nchini Rwanda. Kutoka kushoto: Philippe Mpayimana, Paul Kagame, Frank Habineza.Picha: AFP

Wakati wa chaguzi tatu zilizopita, Kagame alishinda kwa zaidi ya asilimia 93, na mara hii ni wagombea wawili pekee na wasio na ushawishi ndio walioidhinishwa kuchuana naye. Kagame alishikilia nyadhifa za makamu wa rais na waziri wa ulinzi kabla ya kuchaguliwa na Bunge mnamo mwaka 2000 kuwa rais wa nchi hiyo.

Soma pia: Rwanda: Kagame kurejea madarakani kwa muhula wa nne?

Kagame amekuwa akimwagiwa sifa kutoka kwa mataifa ya Magharibi ambayo yalidhamiria kujitakasa kutokana na kushindwa kuchukua hatua wakati wa mauaji hayo na amekuwa akitajwa kama mtu aliyewezesha kuufufua uchumi wa Rwanda  ambapo pato la taifa la limekuwa likikua kwa karibu asilimia nane kila mwaka.  

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 66, amekuwa pia akijaribu kuitangaza vyema Rwanda nje ya nchi kwa kuandaa mikutano, kusaini mikataba ya udhamini na vilabu vikubwa vya soka vya kimataifa na kuonyesha kuwa Rwanda ni kivutio kikuu cha utalii unaoheshimu ikolojia.

Kashfa zinazoukabili utawala wa Kagame

Mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda Victoire Ingabire akitembea nje ya Gereza kuu ya Nyarugenge mara baada ya kuachiliwa huru mnamo Septemba 15, 2018Picha: CYRIL NDEGEYA/AFP

Lakini yote hayo hayawezi kufuta ukweli au kuficha rekodi mbaya ya haki za binadamu zilizoshuhudiwa chini ya utawala wa chama cha Rwandan Patriotic Front (RPF), huku wanaharakati na wapinzani wakimtuhumu Kagame kwa kukandamiza upinzani kwa vitisho, kuwawekwa kizuizini kiholela, kuwateka nyara na hata kuendesha mauaji.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yamekuwa mara kwa mara yakipiga kelele kuhusu ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari na wapinzani wa kisiasa. Tukio la karibuni zaidi ni la mwaka 2020 ambapo shujaa wa filamu ya "Hotel Rwanda" Paul Rusesabagina alikamatwa wakati ndege aliyoamini ilikuwa ikielekea Burundi ilipotua mjini Kigali katika kile familia yake ilisema ni utekaji nyara. Serikali ya Rwanda ilikiri kufadhili operesheni hiyo.

Soma pia: Victoire Ingabire azuwiliwa kugombea urais Rwanda

Mkosoaji huyo mkubwa wa Kagame alihukumiwa kifungo cha miaka 25 jela kwa tuhuma za ugaidi, kabla ya kuachiliwa mwaka jana kufuatia msamaha wa rais uliochochewa na shinikizo la kimataifa. Mwanasheria na mchambuzi wa siasa za Rwanda Louis Gitinywa anasema kuwa chama cha RFP "kinatokomeza uwanja wa kidemokrasia".

Lakini pia Kagame ambaye ni kamanda mkuu wa jeshi ambalo limekuwa na jukumu muhimu la kulinda amani katika mataifa mbalimbali ya Afrika, lakini pia anatuhumiwa kuyumbisha usalama wa nchi jirani ya  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  kwa kuwaunga mkono na kushirikiana bega kwa bega na waasi wa M23, hii ikiwa ni kwa mujibu wa wataalam wa Umoja wa Mataifa.