Paul Pogba ana mambo mengi ya kuonesha
12 Novemba 2016Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps anasisitiza kwamba kuna mambo mengi zaidi katika mchezo wa Paul Pogba baada ya mchezaji huyo wa Manchester United kufunga bao tena katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sweden jana Ijumaa(11.11.2016).
Mchezaji huyo ghali kabisa duniani alifunga kwa kichwa katika ushindi huo wa Ufaransa , ambapo Dimitri Payet aliunga bao la ushindi katika mchezo wa kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia katika uwanja wa Stade de France nchini Ufaransa.
Ni bao la nane la Pogba kwa nchi yake na linafuatiwa na bao la ushindi alilofunga ugenini dhidi ya Uholanzi mwezi uliopita.
Pogba mwenye umri wa miaka 23 pia alifunga bao safi katika ushindi wa mabao 3-1 wa timu yake ya United dhidi ya Swansea katika ligi ya Uingereza Premier League mwishoni mwa juma lililopita lakini Deschamps alisema: "Si mfungaji mabao. Anaweza kufunga mabao na ameweza kufanya hivyo lakini simtarajii kufanya hivyo.
"Ni vizuri alivyofanya leo lakini ninafurahi zaidi kwa jinsi alivyocheza hali ambayo inafuatia mchezo mzuri aliocheza Uhloanzi.
"Kwa Manchester anatumika katika nafasi nyingine katika mfumo tofauti. Alitupa uwezo mkubwa wa kucheza mpira na alikuwa mzuri katika kunyang'anya mipira," Deschamps aliongeza.
"Wakati Paul akicheza kama hivi na anashirikiana vizuri na Blaise Matuidi ni muhimu kwa timu. Iwapo anafunga mabao , ni vizuri zaidi. Nafahamu anapenda kufunga lakini si kitu ambacho mimi pamoja na timu tunakitarajia kutoka kwake."
Ufaransa inaongoza kwa pointi tatu dhidi ya Sweden katika kundi A ikiwa imebakia michezo minne katika duru ya Ulaya ya kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia mwaka 2018 nchini Ufaransa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Sylvia Mwehozi