1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga: Bayern yatoa onyo kwa wapinzani

Admin.WagnerD15 Agosti 2015

Lligi kuu ya Ujerumani Bundesliga imeanza kurindima hapo jana Ijumaa (14.08.2015)ambapo Bayern Munich ikiwa nyumbani na mabingwa watetezi ilifungua pazia kwa kuumana na SV Hamburg

Bundesliga Bayern München gegen SV Hamburg
Bayern Munich wakishangiria baoPicha: Getty Images/AFP/C. Stache

Mabingwa watetezi Bayern Munich walifungua msimu mpya wa Bundesliga kwa kuikandika SV Hamburg kwa mabao 5-0 na kutoa ujumbe mkali kwa timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo kuwa ina nia ya kuweka historia kwa kunyakua taji hilo kwa mara ya nne mfululizo. Bayern ilishinda pambano hilo la ufunguzi usiku wa jana Ijumaa bila ya kuhitaji nguvu za ziada.

Robert Lewandowski , kwa msaada wa mpira uliomgonga mmoja kati ya wachezaji wa Hamburg karibu na lango, alipachika bao la pili dakika nane baada ya kipindi cha pili na wakati huo Hamburg ikiwa haina uwezo tena wa kufanya mashambulizi ya maana , mchezo huo ulikuwa tayari umekwisha amuliwa.

Robert Lewandowski wa Bayern MunichPicha: L. Preiss/Bongarts/Getty Images

Thomas Mueller aliongeza mabao mengine mawili kabla ya mchezaji aliyesainiwa msimu huu Douglas Costa kupigilia msumari wa mwisho katika jeneza la Hamburg usiku wa jana na wakati huo Hamburg ilikuwa inasubiri tu firimbi ya mwisho ili kufikisha mwisho madhila ya.

Wachezaji wapya wapewa nafasi

Kocha wa Bayern Pep Guardiola amewapa nafasi wachezaji waliosajiliwa msimu huu Arturo Vidal na Douglas Costa .

Thomas Mueller wa Bayern MunichPicha: L. Preiss/Bongarts/Getty Images

Costa tangu siku ya kwanza ameweza kujijumuisha vizuri katika timu hii, mkurugenzi wa soka wa Bayern Matthias Sammer amekiambia kituo cha televisheni ya taifa cha ARD.

Mueller na Lewandowski pia wamemwagia sifa tele Mbrazil huyo.

"Ulikuwa mchezo mzuri , tulifurahi pamoja na mashabiki , na tulicheza vizuri." Mueller alisema.

Mchezaji wa kati wa Bayern Arturo VidalPicha: Getty Images/AFP/C. Stache

Hamburg ambayo iliepuka kushuka daraja msimu uliopita kwa kupitia mchezo wa mtoano na timu iliyoshika nafasi ya tatu katika daraja la pili msimu uliopita, ina rekodi mbovu kabisa hivi karibuni dhidi ya Bayern Munich, ambapo ilitandikwa mabao 8-0 na 9-2 katika misimu miwili iliyopita.

Tulipaswa kutuma ishara maalum , hatutaki timu yoyote ifikirie kwamba wanaweza kushindana na sisi," mkurugenzi wa soka wa Bayern Matthias Sammer amesema.

Rekodi ya Hamburg kwa Bayern ni mbaya

Baada ya kukubali mabao 30 katika michezo yake mitano ya ligi walipotembelea Munich , Hamburg ilianza mchezo huo kwa tahadhari , wakitumia walinzi sita na kufunga mianya na maeneo.

Mchezaji mpya wa Bayern Douglas CostaPicha: Getty Images/AFP/C. Stache

"Ilikuwa ngumu , walikuwa wanalinda lango lao lakini tulicheza vizuri kipindi cha pili," amesema kocha wa Bayern Pep Guardiola.

Ligi inaendelea tena leo , wakati Leverkusen inaikaribisha Hoffenheim, Werder Bremen iko nyumbani ikiisubiri Schalke 04. Timu iliyopanda daraja msimu huu Ingolstadt imo njiani kuelekea Mainz , wakati Hannover 96 inasubiriwa na Darmstadt ambayo nayo imeanza kuonja soka la daraja la kwanza msimu huu.

Borussia Dortmund ina miadi jioni ya leo na Borussia Moenchengladbach, wakati makamu bingwa msimu uliopita Wolfsburg itaanza kampeni kesho Jumapili ikiumana na Eintracht Frankfurt.

Bayern Munich dhidi ya Hamburg SVPicha: L. Preiss/Bongarts/Getty Images

Stuttgart ambayo nayo iliponea chupu chupu kushuka daraja msimu uliopita inaikaribisha FC Koln hapo kesho.

Kombe la shirikisho, DFB Pokal

Wakati huo huo kombe la shirikisho duru ya pili limepangwa jana, ambapo mara hii , timu za daraja la kwanza zinapambana na mapema, na vumbi litatimka Oktoba 27 hadi 28 wakati mabingwa watetezi Wolfsburg itakapokabana koo na Bayern Munich , wakati Borussia Moenchengladbach itaoneshana kazi na Schalke 04. Werder Bremen imepangiwa kikosi cha FC Koln .

Mshambuliaji wa Wolfsburg Bas DostPicha: picture-alliance/dpa/P. Steffen

Borussia Dortmund makamu bingwa wa kombe la shirikisho DFB Pokal itaoneshana kazi na paderborn kutoka daraja la pili.

Ligi ya Uingereza Premier League pia itakuwapo uwanjani kesho ambapo Southampton itaumana na Everton, Sunderland inaikaribisha Norwich City, Swansea ina miadi na Newcastle. Stoke City inaifuata Tottenham Hot Spurs nyumbani , wakati Watford iko nyumbani ikiisubiri West Bromwitch Albion. West Ham itakuwa na kibarua dhidi ya Leicester City.

Jumapili ni zamu ya Cristal Palace kukabana koo na Arsenal, wakati pambano la kukata na shoka ni kati ya Manchester City ikiisubiri Chelsea.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre

Mhariri: Daniel Gakuba