1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Pazia la kampeni za uchaguzi mkuu lafunguliwa Rwanda

22 Juni 2024

Pazia la kampeni za uchaguzi wa rais na bunge nchini Rwanda limefunguliwa leo Jumamosi ambapo Rais Paul Kagame anawania kiti hicho kwa mara ya nne.

Rwanda Musanze | mkutano wa ufunguzi wa kampeni| Paul Kagame
Rais Paul Kagame wa Rwanda akiwa kwenye mkutano wa ufunguzi wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Julai 15 uliofanyika katika wilaya ya kaskazini mwa Rwanda ya Musanze.Picha: Jean Bizimana/REUTERS

Katika uchaguzi huo wa Julai 15 Kagame anatarajiwa kurefusha utawala wake wa mkono wa chuma wa miaka 24 kwenye taifa hilo la kanda ya Maziwa Makuu.

Wanyarwanda takribani milioni 9 wameandikshwa kushiriki uchaguzi huo wa urais ambao kwa mara ya kwanza utafanyika sambamba na ule wa bunge.

Akizungumza kwenye mkutano wa ufunguzi wa kampeni uliohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wake, wengi wakiwa wamefikishwa hapo kwa mabasi, Kagame ametetea rikodi ya nchi yake kwenye suala la demokrasia. Matamshi yake yanalenga kuwafunga midomo wale wanaoutuhumu utawala wake kwa kukandamiza upinzani na kutawala na mabavu.

"Kwa kawaida watu hutofautiana kuhusu demokrasia au huielewa dhana hiyo kwa namna tofauti. Lakini kwetu sisi, tunayo tafsiri yetu ya (demokrasia). Demokrasia maana yake ni kuwepo chaguo, kuchagua kati ya kizuri kwako na kile unachokitaka," amesema Kagame huku akishangiliwa na umma uliokusanyika kwenye mji wa kaskazini mwa Rwanda wa Musanze.

"Hakuna kitu bora zaidi ya kuwa Mnyarwanda, lakini ni muhimu zaidi, ni mimi kuwa kiongozi wenu ... nimekuja hapa kuwashukuru, siyo kuomba kura zenu."

Kagame kuchuana na wanasiasa wawili, wengine wapigwa kufuli 

Katika uchaguzi wa mwaka huu Kagame anachuana na wapinzani wawili ambao pia waliwania nafasi hiyo katika uchaguzi uliopita wa 2017.

Wagombea urais Rwanda kutoka kushoto Philippe Mpayimana, Paul Kagame na Frank Habineza.Picha: AFP

Wapinzani hao ni Frank Habineza kutoka chama cha Democratic Green na mwandishi wa habari wa zamani Philippe Mpayimana, anayeshiriki kama mgombea binafsi.

Mahakama za Rwanda zilikataa rufaa za wanasiasa vigogo wa upinzani  Bernard Ntaganda na Victoire Ingabire za kuwafutia hatia walizokutwa nazo miaka ya karibuni ambazo kwa sheria za nchi hiyo zinawazuia kuwania kitu cha urais.

Tume ya Uchaguzi pia ilimpiga marufuku mkosoaji mkubwa wa Kagame, Diane Rwigara ikisema ameshindwa kutoa nyaraka zinazoonesha rikodi yake ya uhalifu kama inavyotakiwa kisheria na kwamba hakutimiza takwa la kukusanya saini 600 za raia wanaomuunga mkono.

Diane, mtoto wa tajiri Assinapol Rwigara aliyekuwa mfadhili mkubwa wa chama cha Kagame cha RPF hadi walipotumbukia kwenye msuguano, alikamatwa na kuzuiwa kugombea urais mwaka 2017 kwa madai ya kughushi nyaraka. Hata hivyo baadaye mashtaka hayo dhidi yake yalifutwa.

Kagame na sifa za mageuzi ya kiuchumi chini ya kivuli cha ukandamizaji 

Rais Kagame amekuwa amekuwa mtawala wa Rwanda mtu angeweza kusema tangu baada ya kukomeshwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambayo yaliwaangamiza karibu watu 800,000 wengi kutoka jamii ya Watutsi na vilevile Wahutu wenye misimamo ya wastani.

Maelfu ya wafuasi wa rais Paul Kagame wamehudhuria mkutano wa kwanza wa kampeni katika wilaya ya Musanze.Picha: Jean Bizimana/REUTERS

Aliingia madarakani rasmi kuwa rais mwaka 2000 kwa kuchaguliwa na bunge baada ya kujiuzulu kwa rais Pasteur Bizimungu.Tangu wakati huo ameshinda chaguzi tatu kwa zaidi ya asilimia 90 mnamo mwaka 2023, 2010 na 2017. Katika uchaguzi wa mwisho wa mwaka 2017, Kagame alijizolea asilimia 99 ya kura.

Kiongozi huyo amekuwa akipata sifa kwenye jukwaa la kimataifa kwa kufanya maguezi makubwa ya kiuchumi nchini Rwanda baada ya mauaji ya kimbari lakini anaandamwa na ukosoaji wa kila wakati kuhusu rikodi dhaifu ya haki za binadamu na ukandamizaji wa kisiasa.

Katika taarifa iliyotolewa wiki iliyopita, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeituhumu serikali kwa kufanya ukandamizaji wa muda mrefu dhidi ya upinzani, vyombo vya habari na asasi za kiraia.

"Kitisho cha kushambuliwa kimwili, kesi zinazoendeshwa kwa hila, na hukumu za kifungo cha muda mrefu jela vimewanyamazisha Wanyarwanda wengi kushiriki katika shughuli za kisiasa na kuwawajibisha viongozi wao," alisema  Clementine de Montjoye mtafiti mwandamizi wa HRW kanda ya Afrika.  

Mwaka 2015, Kagame alisimamia mchakato wa mabadiliko ya katiba yaliyofungua njia ya yeye kuendelea kutawala hadi mwaka 2034.

Uchaguzi wa bunge mara hii utahusisha zaidi ya wagombea 500 huku wakipakura wakiwachagua wabunge 53 katika bunge la viti 80.

Nafasi nyingine 27 zinazosalia ni za makundi maalumu ikiwemo 24 wanawake, wawakilishi wawili wa vijana na nafasi moja ya mbunge kutoka kundi la watu wenye ulemavu.