1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Peer Steinbrück ashika kani

Abdu Said Mtullya20 Septemba 2013

Mgombea ukansela wa SPD Peer Steinbrück ni mtu mwerevu,mwenye uwezo wa kujieleza na mtaalamu wa masuala ya fedha.Licha ya kura za maoni kuonyesha kwamba yupo nyuma, anaamini kuwa ataweza kushinda uchaguzi.

Mgombea ukansela wa chama cha SPD Peer Steinbrück
Mgombea ukansela wa chama cha SPD Peer SteinbrückPicha: picture-alliance/dpa

Mgombea ukansela wa chama cha Social Demokratik SPD Peer Steinbrück ameshika kani na amesimama imara. Steinbrück siyo mwanasiasa wa kuzunguka anapozungumza,Anaposimama kwemye mimbari ,anazungumza wazi wazi. "Nataka kuwa Kansela wa Ujerumani"

Atokea katika familia ya wafanya biashara

Steinbrück anaetokea katika familia ya wafanyabiashara kutoka mji wa Hamburg amekuwamo katika shughuli za kisiasa katika chama cha SPD kwa miongo mingi. Baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu katika taaluma ya uchumi alianza kazi ya kuwa mshauri maalumu kwenye ofisi ya Kansela.Baada ya hapo alitumikia nyadhifa mbalimbali kwenye taasisi na wizara. Steinbrück aliwahi kuwa Waziri wa fedha na Waziri Mkuu wa jimbo la Northrhine Westphalia kuanzia mwaka wa 2002 hadi mwaka wa 2005. Lakini hakuchaguliwa tena kuwa Waziri mkuu.Mnamo mwaka wa 2005, chama chake kilimpendekeza kuwa waziri wa fedha katika serikali ya mseto mkubwa iliyoongozwa na Kansela Angela Merkel.

Amgeukia Merkel

Pamoja na Kansela Merkel Steinbrück alijaribu kuukabili mgogoro wa fedha.Lakini leo Steinbrück amemgeukia Merkel na kusema kuwa Kansela huyo ametawala tu badala ya kujenga. Steinbrück amesema kwamba kwa kiwango kikubwa ustawi wa uchumi nchini Ujerumani unatokana na mpango wa chama cha SPD. Mwanasiasa huyo anadhamiria kujitambulisha kama mtendaji na mjengaji.Lakini pana tatizo moja.

Kabla ya chama chake cha SPD kumteua kuwa mgombea ukansela mnamo mwaka wa 2012,Steinbrück ,wakati akiwa mbunge wa kawaida alilipwa fedha nyingi kutoka sehemu kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoka kwenye mabenki.Alilipwa kwa kutoa mihadhara juu ya masuala ya fedha. Alilipwa zaidi ya Euro milioni moja.Wapinzani wake wa siasa na wananchi kadhalika wanauliza vipi mgombea ukansela anaweza kuaminika ikiwa amelipwa fedha nyingi na mabenki lakini wakati huo huo anayashutumu mabenki kwa uroho na wakati ambapo anapiga kelele juu ya kasoro zilizopo katika jamii?. Lakini kwenye mkutano wa kampeni ya uchaguzi mkewe alimtetea kwa kusema kwamba Steinbrück ni mtu wa kuaminika.

Atoa machozi

Hata hivyo alipoulizwa na mwandishi habari mmoja kwa nini anataka kuwa Kansela Steinbrück alikwama na alianza kutoa machozi. Lakini baada ya muda mfupi Steinbrück alirejea katika hali yake ya kawaida. Yeye ni mtu mwenye busara na mwerevu lakini wakati mwingine pia ana machachari, anatabia ya kuwasomesha watu na pia wakati mwingine ni mpungufu wa diplomasia.

Hata hivyo anatetea sera ya haki. Steinbrück amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni utajiri wa watu binafsi umekuwa unaongezeka. Matajiri wanazidi kutajirika hali masikini wanazidi kuwa masikini.Ndiyo sababu anataka sehemu ya utajiri huo wa watu binafsi utozwe kodi kwa manufaa ya jamii.Mapato hayo ya kodi yaekezwe katika elimu,ujenzi wa miundo mbinu, na yatumike kwa ajili ya kulipunguza deni la nchi na pia yatumike kwa ajili ya kuziimarisha serikali za mitaa.

Ataka Uturuki iwemo katika Umoja wa Ulaya

Juu ya sera za nje Steinbrück anaunga mkono Uturuki kuingizwa katika Umoja wa Ulaya na anaitaka Urusi iheshimu haki za binadamu. Steinbrück pia anataka sera ngumu ya Umoja wa Ulaya ya kubana matumizi ilegezwe katika nchi masikini za kusini mwa Ulaya.Lakini wakati huo huo anasisitiza juu ya umuhimu wa mageuzi katika nchi hizo.

Mwandishi:Dick,Wolfgang

Tafsiri:Mtullya Abdu.

Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW