Peer Steinbrück kupigania kiti cha kansela kwa tikiti ya SPD
1 Oktoba 2012Tuanzie Berlin ambako chama cha SPD, kwa kumteuwa waziri wa zamani wa fedha Peer Steinbrück kimepania kurejea madarakani uchaguzi mkuu utakapoitishwa september au oktober mwakani.Lakini wahariri wanaiangalia vipi dhamiri hiyo?Gazeti la "Der neue Tag" linaandika:
Msimamo bayana wa Peer Steinbrück dhidi ya ule wa tahadhari wa kansela Angela Merkel una kikomo.Miezi 12 ya ukweli wenye shubiri inaweza kuwatisha wapiga kura.Na ulimi mkali unaweza kugeuka tusi kama ule mkasa unaomfika Mitt Romney hivi sasa.Peer Steinbrück na SPD wanajikuta ukingoni mwa njia.
Gazeti la "Saarbrücker Zeitung" linajaribu kufafanua kwanini SPD wamemchagua Peer Steinbrück na sio Frank-Walter Steinemeier ashindane na kansela Angela Merkel katika uchaguzi mkuu mwakani.Gazeti linaendelea kuandika:
SPD wanataka katika kipindi cha miezi hii iliyosalia,warejeshe imani ya wapiga kura wote wale waliowapoteza kwasababu ya Agenda 2010 na kujiunga ama na mrengo wa shoto au na kundi la wanaogoma kupiga kura.Lakini Steinbrück hatosaidia kitu kwasababu moyo wa wengi kati ya waliovunjwa moyo unapiga zaidi mrengo wa shoto.Mwenyekiti wa chama,Sigmar Gabariel atabidi awajibike ili Steinbrück aweze kama anavyosema "kujifaragua" na kuweza kuutetea mtindo wake wa kisiasa."
Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha pia na uchaguzi wa Marekani.Gazeti la "Emder Zeitung limeandika kuhusu mjadala utakaofanyika kati ya wagombea wawili na kushadidia nafasi ya rais anaemaliza wadhifa wake Barack Obama.Gazeti linaebndelea kuandika:
Obama anaweza bila ya taharuki kujibwaga mashindanoni.Uchunguzi wa maoni ya umma unaonyesha atashinda.Hali hiyo haisababishwi na sera zake,bali na udhaifu wa yule anaeshindana nae.Obama anaweza kupumua,kutokana na kupwaya mpinzani wake.Kauli mbiu aliyoipigia upatu miaka minne iliyopita "Ndio tunaweza" ,haijasalia kitu.Vikosi vya Marekani bado viko nchini Afghanistan,idadi ya wasiokuwa na kazi bado ni ya juu,na katika suala la ulinzi wa mazingira hakuna chochote kilichofanyika.Matarajio ya juu aliyowekewa mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel Obama,hayakutekelezwa.
Mada ya mwisho inahusu maandamano dhidi ya hatua za kufunga mkaja nchini Hispania na Ureno.Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linaandika:
Ni dhahir kwamba subira ya wakaazi wa ghuba ya Iberia imefikia kikomoni.Hisia za watu kuvunjika moyo zinazidi kuongezeka.Na hali hiyo ni ya tangu zamani.Kwasababu wahispania na wareno,hawaoni dalili ya mabadiliko licha ya hatua za kufunga mkaja.Zaidi ya hayo wananchi wa Hispania na Ureno wameshochwa na serikali za kihafidhina ambazo uchunguzi wa maoni ya umma unaonyesha umashuhuri wao unazidi kuporomoka.Na kwa namna hiyo serikali hizo hazitakuwa na kazi rahisi kutekeleza mageuzi yaliyokusudiwa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Yusuf Saumu