1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasiasa Ujerumani watahadharisha juu ya hatari ya Pegida

Admin.WagnerD20 Oktoba 2015

Wanasiasa nchini Ujerumani wameeleza kwamba kundi la watu wanaopinga kusilimishwa kwa bara Ulaya,"PEGIDA" linaeneza chuki, na wanataka hatua zichukuliwe ili kuwakabili watu hao.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de MaizierePicha: Getty Images/S. Gallup

Watu wa Pegida hapo jana walifanya maandamano makubwa katika mji wa Dresden kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa kundi lao.

Wanasiasa wa Ujerumani wametoa tahadhari hiyo baada ya Meya wa mji wa Cologne, Henriette Reker kuchomwa kisu, na baada ya watu wa Pediga kufanya maandamano makubwa katika mji wa Dresden mashariki mwa Ujerumani.

Kwa mujibu wa taarifa,ghasia zilitokea baada ya wananchi wengine kufanya maandamano sambamba ya kuwapinga watu hao wanaowapinga wageni na Waislamu .Wasemaji wa kundi la Pegida wamearifu kwamba watu kati ya 15,000 na 20,000 walishiriki kwenye maandamano ya mjini Dresden.

Picha: DW

Watu kati ya15,000 na 19,000 waliojitokeza kuwapinga wabaguzi hao walikusanyika kwenye sehemu mbalimbali na kutoa kauli mbiu iliyosema "upendo badala ya chuki." Katika ghasia zilizotokea, wafuasi wa kundi la watu wanaoupinga Uislamu barani Ulaya waliwatupia polisi fataki.

Gazeti moja la jimbo la Saxony limeripoti kwamba mfuasi mmoja wa Pegida alijeruhiwa kutokana na kushambuliwa na chuma lakini gazeti hilo halikutoa habari zaidi.

Waziri asema Pegida ni jumuiya ya siasa kali

Akitahadharisha juu ya hatari ya kundi la Pegida, Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesema sasa wamo katika hatua ya kujaribu kubainisha iwapo kundi la Pegida ni la itikadi kali. Lakini amesema sasa ni wazi kabisa kwamba wale wanaoliongoza kundi hilo ni watu wenye siasa kali.

Msemaji wa polisi wa mji wa Dresden amearifu kwamba ghasia ziliendelea jana usiku ambapo wananchi wanaowatetea wakimbizi walipambana na wafuasi wa Pegida.

Wakati huo huo ripota wetu wa DW Jafaar Abdul Karim alifanyiwa fujo na wafausi wa Pegida alipokuwa anaripoti juu ya maandamano. Abdul Karim na wenzake wengine wawili walizingirwa na watu wa Pegida na walizuiwa kufanya kazi yao

Mkurugenzi mkuu wa DW Peter Limbourg ameilaani kadhia hiyo na amesema hatua za kisheria zitachukuliwa.

Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Juu ya maandamano ya Pegida msemaji wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameeleza kuwa Kansela huyo anaamini kwamba wafuasi wa Pegida walioshiriki kwenye maandamano ya mjini Dresden wamejawa chuki katika nyoyo zao.

Kansela Merkel aliwataka watu wajiweke mbali na maandamano ya Pegida.

Kundi la Pegida ambalo hadi hivi karibuni liliwapoteza wanachama wake wengi, sasa limepata nguvu upya.

Wanasiasa kadhaa wametoa mwito kwa wanaanchi wa Ujerumani wawe na ujasiri wa kujitokeza na kuwakabili wanaoeneza chuki.

Kiongozi wa chama cha watetezi wa mazingira -chama cha kijani, Katrin Göring amesema anaelewa kuwa watu wana wasi wasi na hofu lakini amesema chuki siyo jambo sahihi.

Mwandishi:Mtullya Abdu./ZA dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman