PEKING: Madai ya Pyongyang yachelewesha maafikiano
11 Februari 2007Matangazo
Hakuna ishara kuwa maendeleo yamepatikana katika majadiliano ya kundi la pande sita mjini Beijing, kuhusu mradi wa nyuklia wa Korea ya Kaskazini. Majadiliano hayo yakiendelea kwa siku ya nne,kuna ripoti zinazogongana,kama wajumbe hao wanakaribia kuafikiana.Kwa mujibu wa mjumbe wa Marekani, Christopher Hill,maendeleo makubwa yamepatikana na ni suala moja tu linalochelewesha maafikiano, lakini hakueleza zaidi.Kwa upande mwingine,mjumbe wa Japan katika majadiliano hayo,Kenichiro Sasae amesema,tatizo kuu ni madai ya serikali ya Pyongyang inayotaka misaada mikubwa mbali mbali. Kundi hilo la pande sita ni Korea ya Kaskazini, Japan,Marekani,China,Urussi na Korea ya Kusini.