Pelosi amwuunga mkono Dalai Lama
21 Machi 2008Spika wa baraza la wawakilishi nchini Marekani Nancy Pelosi ameitaka jumuiya ya kimataifa ishutumu utawala wa China katika jimbo la Tibet na hatua inazochukua dhidi ya wapinzani.
Pelosi amesema hayo leo baada ya kukutana na kiongozi wa kidini wa Tibet Dalai Lama mjini Dharamshala,kaskazini mwa India.
Bibi Pelosi ni mwanasiasa wa kwanza wa ngazi za juu kutoka Marekani kukutakana na Dalai Lama tokea ghasia zifumuke katika jimbo la Tibet wiki iliyopita.
Spika Pelosi amekutana na Dalai Lama wakati ambapo China na viongozi wa upinzani wa Tibet wanabishana juu ya idadi ya watu waliokufa kutokana na ghasia hizo.Idara za serikali za China zimesema maafisa wake waliwapiga risasi na kuwajeruhi wapinzani wanne mwishoni mwa wiki, na inawalaumu wapinzani hao kwa kuwaua raia 13 baada ya ghasia kutokea ijumaa iliyopita katika mji wa Lhasa ndani ya Tibet.Lakini wawakilishi wa upinzani wa Tibet wanaoishi nje wamesema watu wapatao mia moja wameuliwa na polisi wa China tokea machafuko hayo yaanze.
Akizungumzia hali ya jimbo la Tibet spika wa baraza la wawakilishi la Marekani bibi Pelosi amesema ikiwa jumuiya ya kimataifa haitasema chochote juu ya utawala wa China katika Tibet, basi dunia itakuwa imepoteza uadilifu wote juu ya suala la haki zabinadamu.
Lakini kiongozi wa kidini wa Tibet mwenyewe Dalai Lama amesema pamoja na kuungwa mkono kutoka nje,
suluhisho linapaswa kufikiwa baina ya China na wawakilishi wa Tibet.
Wakati huo huo China imekiri kwa mara ya kwanza kuwa maafisa wake wa usalama waliwashambulia wapinzani wa Tibet kwa risasi wakati wanajeshi wake leo wameendela na msako katika sehemu kadhaa huku kukiwa na wasi wasi juu ya wapinzani zaidi kutiwa ndani.