1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pelosi asema Marekani haitaitelekeza Taiwan

3 Agosti 2022

Spika wa baraza la wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi ameondoka Taiwan na kusema kwamba yeye na wabunge wengine katika ujumbe wake wameoneesha kuwa hawataacha kujitolea kwao katika kisiwa cha Taiwan kinachojitawala.

Taiwan Taipei | Nancy Peolosi und Tsai Ing-wen
Picha: Taiwan Presidential Office/REUTERS

Pelosi, spika wa kwanza wa bunge la Marekani kukitembelea kisiwa hicho kwa zaidi ya miaka 25, alitaja ghadhabu ya China kutokana na ziara hiyo na kuanzisha mjadala wa zaidi ya wiki kuhusu iwapo lilikuwa wazo zuri baada ya habari hizo kuvuja.

Wakati wa mkutano wa pamoja na wanahabari akiwa na rais wa Taiwan Tsai Ing-wen, Pelosi amesema kuwa dunia kwa sasa inakabiliwa na chaguo kati ya demokrasia na udikteta na kuongeza kuwa kujitolea kwa Marekani kudumisha demokrasia nchini Taiwan na kote duniani bado kuko thabiti.

Pelosi asema Marekani ilitoa ahadi kwa Taiwan

Pelosi ameongeza kusema miaka 43 iliyopita, na sheria ya ushirikiano na Taiwan, Marekani ilitoa ahadi thabiti ya kusimama na Taiwan kila wakati. Na kutokana na msingi huo imara, wamejenga ushirikiano unaostawi katika misingi ya maadili ya pamoja ya kujitawala na kujitolea kwa kulenga maslahi ya pamoja ya usalama katika kanda hiyo na kote ulimwenguni, kujitolea kwa ushirikiano wa kiuchumi ambao utawezesha ustawi wa watu wote.

Rais wa China Xi JinpingPicha: Huang Jingwen/Xinhua News Agency/picture alliance

Wakati wa mkutano huo na wanahabari Tsai alisema kuwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umeangazia wasiwasi wa kiusalama kuhusu Taiwan. Tsai ameonya kuwa uvamizi dhidi ya taifa hilo la kidemokrasia utakuwa na athari mbaya katika usalama wa kanda nzima ya Indo-Pasifiki.

Kabla ya kuondoka Taiwan, Pelosi alikutana na wanaharakati wa haki za binadamu mjini Taipei akiwemo kiongozi wa zamani wa vuguvugu la demokrasia nchini China Wu'er Kaixi, ambalo lilikandamizwa kwa umwagikaji damu mnamo 1989. Pelosi pia alikutana na Lam Wing-kee muuzaji vitabu wa zamani na mwanaharakati wa kijamii Ming -chee wote ambao walikuwa wamefungwa nchini China katika bustani ya haki za binadamu na utamaduni ya Jingmei kusini mwa Taipei. Lee alikuwa amerejea tu Taiwan kutoka China baada ya kutumikia kifungo cha miaka mitano jela kwa kuhujumu nguvu ya serikali.

China yatangaza mazoezi ya kijeshi karibu na Taiwan

China ambayo inadai kuwa Taiwan ni sehemu ya himaya yake na kupinga ushirikiano wowote wa maafisa wa Taiwan na serikali za kigeni, imetangaza mazoezi mengi ya kijeshi karibu na kisiwa hicho, ambayo kwa sehemu yataingilia bahari ya Taiwan na pia kutoa mfululizo wa matamshi makali baada ya ujumbe huo wa Marekani kuwasili Jumanne usiku katika mji mkuu wa Taiwan, Taipei.

Taiwan imelalamika kuhusu hatua hizo zilizopangwa na kusema zinakiuka uhuru wa kisiwa hicho

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW