Penalti tano zakosa nyavu Bundesliga wiki hii
17 Oktoba 2016Ilikuwa wiki ya saba ya Bundesliga ambayo wachezaji kadhaa walishindwa kutumbukiza mipira ya penalti wavuni, haijawahi kutokea katika historia ya kandanda la Bundesliga.
Kulikuwa na penalti tano kwa jumla katika michezo ya mwishoni mwa juma ya Bundesliga na yote ilipotea bila kutumbukia wavuni. Emil Forsberg wa RB Leipzig alikuwa wa mwisho katika jumla ya wapigaji kukosa penalti yake dhidi ya Wolfsburg jana Jumapili. lakini hata hivyo raia huyo wa Sweden aliweza kutandika mkwaju kutoka mita 20 na ukaleta faraja kwa Leipzig kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wolfsburg ambayo hadi sasa imepata ushindi mara moja sare tatu na kushindwa mara tatu.
Huyu hapa Emil Forsberg mfungaji wa bao hilo.
"Ni rahisi tu, tunajituma sana na tunajiamini sana na tunajua kwamba tunaweza. Tunatambua , kwamba tunaweza kushinda dhidi ya timu yoyote. Ninajivunia timu yetu."
Hali hiyo lakini imeiweka Wolfsburg katika hali ngumu. Wolfsburg kwa mara nyingine imeshindwa, na haijaweza kuweka mpira katika nyavu za adui. Wlfsburg imeteleza kwenda chini zaidi na kutumbukia katika matatizo. Tangu timu hiyo ilipopata mafanikio dhidi ya Augsburg , imeambulia tu pointi tatu baada ya kutoka sare bila kufungana na timu ilizokumbana nazo. Matokeo hayo ni maafa kwa Wolsburg , timu ambayo ilifikia katika awamu ya mtoano ya Champions League msimu uliopita. Timu hiyo kwa sasa iko katika nafasi ya 14, ikiwa pointi mbili tu kutoka eneo la hatari la kushuka daraja. Kocha Dieter Hecking ametumbukia sasa katika ukosoaji mkubwa , licha ya kuiongoza timu hiyo kushinda kombe la Ujerumani, DFB Pokal mwaka 2015.
RB Leipzig ni timu iliyoundwa mwaka 2009 , lakini imeibuka na kupita katika ngazi mbali mbali kutoka daraja la nne katika muda wa miaka saba na kufikia katika Bundesliga.
Kikosi chake cha chipukizi watupu , ambacho hakina majina makubwa , kinakonga nyoyo za mashabiki ambao hawana upande kwa kusakata kandanda safi linalopendeza machoni.
Pamoja na viongozi wa ligi hiyo bayern Munich , FC Kolon iliyoko katika nafasi ya pili pamoja na Hoffenheim ambayo iko nafasi ya sita , Leipzig ni moja kati ya timu chache ambacho hazijapoteza mchezo katika ligi ya Ujerumani msimu huu.
Licha ya kuongoza ligi , mabingwa watetezi Bayern Munich wanaonekana kuyumba msimu huu , na hali hiyo imesababisha matamshi makali kutoka kwa mwenyekiti wa klabu hiyo Karl-Heinz Rummenigge ambaye amesema ni hali isiyokubalika kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Eintracht Frankfurt ambayo ilikuwa na wachezaji 10 uwanjani. Bayern haijapata ushindi katika michezo yake mitatu iliyopita.
Huyu hapa mshambuliaji wa Bayern Munich Arjen Robben.
"Kipindi cha mzozo? hilo halina nafasi ya mjadala kwa sasa. Tawimu lakini hazidanganyi. Michezo mitatu ya hivi karibuni hatukuweza kushinda. Inakera , hali hiyo si nzuri. Na pia haikuwa lazima. Haipaswi kabisa kutokea, kwamba unaongoza kwa mabao 2-1 dhidi ya watu 10, na kwamba bado wanapata nafasi ."
FC Kolon inaogelea kwa sasa katika bahari ya ushindi baada ya kuitandika FC Ingolstadt kwa mabao 2-1 nyumbani na kuchupa hadi nafasi ya pili kutoka juu ya kilele cha ligi. Nini siri ya mafanikio ya FC Kolon msimu huu, na nini matarajio ya klabu hiyo kongwe katika Bundesliga, ikiwa ndio mabingwa wa kwanza wa Bundesliga ilipoanzishwa mwaka 1963. Huyu hapa kocha anayeleta mafanikio Peter Stoger.
"Pointi tulizonazo na hali ilivyo, tunataka kuiendeleza , na hatutaki kupunguza kasi. Ni kazi zetu, kutimiza wajibu wetu kutokana na matarajio yanayoongezeka."
Katika michezo mingine TSG Hoffenheim iliendelea kuwa moja kati ya timu ambayo hazijapoteza mchezo kwa kuishinda Freiburg kwa mabao 2-1, Schalke 04 ikatosheka na sare ya bao 1-1 dhidi ya FC Augsburg licha ya kumpoteza mshambuliaji wake mahiri Breel Embolo ambaye ameumia mguu na atakuwa nje ya uwanja huenda kwa mwezi mzima. Borussia Moenchengladbach iliambulia sare ya bila kufungana nayo na Hamburg SV. na Werder Bremen ilionesha kuwa inaanza kubadilika chini ya kocha mpya Alexander Nurri kwa kuishinda Bayer Leverkusen kwa mabao 2-1 .
Mchezaji wa kati wa Werder Bremen Zlatan Junuzovic anasema ushindi huo ulikuwa muhimu sana.
"Ilikuwa muhimu sana, kwamba tumepata pointi tatu kutoka kwa timu ngumu kama hii. Inaonesha kwamba tuna uwezo, lakini tunapaswa kufanyakazi zaidi na tucheze kama timu uwanjani, hilo ni muhimu. Kila mmoja wetu, atakayecheza na wale walioko benchi , kila mmoja awe tayari. Ni hivyo tu tunaweza kushinda mchezo."
Katika ligi nchini Uingereza Premier League , jana Jumapili Middlesbrough ilipinduliwa chali na Watford kwa kuchapwa bao 1-0, wakati Southampton iliicharaza Burnley kwa mabao 3-1. Arsenal inashikilia nafasi ya pili sasa katika msimamo wa ligi ya Uingereza ikiwa na pointi sawa na viongozi wa ligi hiyo Manchester City , baada ya kuishindilia Swansea kwa mabao 3-2 , Bournemouth iliikandika Hull City mabao 6 - 1, Chelsea ikairarua Leicester mabingwa watetezi wa ligi hiyo kwa mabao 3-0. Manchester City ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Everton.
Lakini leo jioni uwanja wa Anfield road utachimbika wakati mafahali wawili Liverpool na Manchester United watakapoooneshana kazi katika mchezo mwingine wa Premier League.
Ushindi dhidi ya manchester United leo utamaliza kumbukumbu chungu za Liverpool kushindwa na kikosi cha kocha wa zamani wa Chelsea Jose Mourinho miaka miwili iliyopita, amesema hivyo mchezaji wa kati Jordan Henderson.
Kocha wa zamani wa Chelsea Mourinho aliiongoza klabu hiyo ya mjini London katika ushindi wa mabao 2-0 katika Premier League uwanjani Anfield Aprili mwaka 2014 na kukatisha ndoto za Liverpool za kupata ubingwa wake wa kwanza wa ligi hiyo tangu mwaka 1990, na hatimaye Manchester City kutawazwa mabingwa.
"Ni kocha wa kiwango cha juu na ameonesha uwezo huo katika vilabu alivyovifundisha," Henderson alisema hayo kuhusu Mourinho , ambae sasa ni meneja wa timu ya Manchester United.
Champions League
Champions League inarejea tena uwanjani kesho Jumanne na Jumatano , ambapo Borussia Dortmund ambayo imeelemewa na majeruhi ikiteremka katika uwanja wa Sporting Lisbon , katika mpambano ambao unaonekana kuwa kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya pili nyuma ya Real Madrid katika kundi gumu la F. Real Madrid iko nyumbani ikiisubiri Legia Warsaw ya Poland timu ya kwanza kutoka Poland kufikia awamu hii katika muda wa miaka 20 iliyopita. Legia Warsaw tayari imebugia mabao nane katika michezo miwili na maporomoko ya magoli yanatarajiwa katika mchezo huo dhidi ya Real Madrid.
Real Madrid imejipasha joto kwa ajili ya pambano hili kwa kuitwanga Real Betis kwa mabao 6-1 , timu ambayo ni bora zaidi kuliko Legia Warsaw.
Katika kundi E Bayer Leverkusen ya Ujerumani inaisubiri Tottenham Hotspurs ya Uingereza. Kipigo ilichopata Tottenham dhidi ya Monaco katika mchezo wa kwanza kimeleta hamasa kubwa katika kundi hili , kwa kuziweka Tottenham na Leverkusen katika mbinyo wakati zikiingia katika mpambano huo.
Spurs ilifanikiwa kurekebisha mambo ilipopambana na CSKA Moscow , lakini Leverkusen haijashinda mchezo hadi sasa katika kundi lake.
CSKA Moscow ni wenyeji wa Monaco.
Michezo mingine ni ya kundi G, ambapo Club Brugge inaisubiri FC Porto ya Ureno na mabingwa wa Uingereza Leicester ina miadi na Copenhagen ya Denmark. Dinamo Zagreb inatoana jasho na Seville ya Uhispania na Lyon ya Ufaransa ni wenyeji wa Juventus Turin ya Italia katika kundi H.
Michezo hiyo itaendelea tena Jumatano ambapo Bayen Munich ya Ujerumani inapambana na Eindhoven ya Uholanzi , Celtic inawasbiri Borussia Moenchengladbach ya Ujerumani , Atletico Madrid inakwenda kucheza na Rostov ya Belarus na barcelona iko nyumbani ikiisubiri Manchester City ya Uingereza, mchezo utakaoikutanisha timu hiyo ya katalani na kocha wake wa zamani Pep Guardiola.
Bafana Bafana
Na chama cha kandanda nchini Afrika kusini kimesema leo kwamba nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo Bafana Bafana Neil Tovey yuko katika hali mbaya baada ya kuugua kiharusi, mara ya pili katika muda wa miaka miwili. Tovey alikuwa nahodha wa bafana bafana katika wakati ambapo timu hiyo ilionesha kiwango cha juu kabisa cha mchezo kwa kunyakua kombe la mataifa ya Afrika. Alipata kiharusi wakati wa mazowezi jana Jumapili. Tovey mwenye umri wa miaka 54 ni mkurugenzi wa ufundi wa shirikisho la kandanda la Afrika kusini.
Kenya imemteua mchezaji wa zamani wa mchezo wa rugby nchini humo Innocent Simiyu kuwa kocha mpya wa timu ya taifa. Simiyu mchezaji wa zamani wa timu ya taifa anachukua nafasi ya Benjamin Ayimba kwa mkataba wa miaka miwili, na amepewa jukumu la kuiongoza Kenya katika mchezo wa kwanza wa kundi la timu saba katika michezo ya dunia ya mwaka 2017 Dubai Desemba mwaka huu.
Richard Omwela mwenyekiti wa chama cha mchezo wa Rugby nchini Kenya , aliwaambia waandishi habari , kwamba Simiyu alipata nafasi ya juu katika usaili , na ndipo alipoteuliwa kuwa kocha wa taifa.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre / ape
Mhariri: Mohammed Khelef