Pence aionya Korea kaskazini
18 Aprili 2017Pence alizungumza kwa maneno makali wakati akianza mazungumzo na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe pamoja na viongozi wengine wa Japan baada ya kuwasili katika kituo cha jeshi la Marekani akitokea Korea kusini.
"Tunatambua hali ngumu ambayo watu wa Japan wanapitia kutokana na uchokozi unaofanywa kutoka upande wa pili wa bahari ya Japan," Pence amesema , na kuongeza "tuko nanyi kwa asilimia 100."
Utawala wa rais Donald Trump umeashiria kuchukua mtazamo wa nguvu zaidi kutokana na majaribio ya hivi karibuni ya makombora ya Korea kaskazini na vitisho, ikiwa ni pamoja na onyo kutoka kwa Trump kwamba kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un, anapaswa , "awe na adabu."
Jana Jumatatu , Pence alisafiri kwenda katika eneo ambalo limetengwa bila kuwa na shughuli za kijeshi , linalotenganisha Korea kaskazini na kusini , ambako alimuonya kiongozi wa Korea kaskazini kwamba baada ya nchi hiyo kuijaribu Marekani na Korea kusini kwa dhamira yake ya kujipatia silaha za kinyuklia, "enzi za mkakati wa uvumilivu zimekwisha."
Marekani yaitaka China kutumia ushawishi wake
Pence akiwa katika ziara ya siku 10 ya mataifa ya Asia ambayo pia itamfikisha nchini Indonesia na Australia , amesema Trump ana matumaini China itatumia ushawishi wake kuwezesha mshirika wake huyo wa karibu kuachana na dhamira yake ya mpango wa kinyuklia. Abe kwa upande wake amesema anamatumaini ya mazungumzo ya amani na Pyongyang, lakini wakati huo huo akaongeza , mazungumzo kwa nia ya mazungumzo tu hayana maana.
"Ni dhahiri kwamba, hili ni suala la umuhimu wa juu kabisa kwetu kutafuta juhudi za kidiplomasia pamoja na suluhisho la amani la suala la Korea kaskazini. Lakini wakati huo huo , mazungumzo kwa ajili tu ya mazungumzo hayana maana na ni muhimu kwetu kuweka mbinyo dhidi ya Korea kaskazini ili iweze kujitokeza na kufanya mazungumzo yenye maana."
Waziri wa mambo ya kigeni wa China Wang Yi ametoa wito mpya leo wa utulivu katika rasi ya Korea. Wang amewaambia waandishi habari kwamba licha ya kuwa maafisa wa Marekani wameweka wazi kwamba shambulio la kijeshi linawezekana, anamini kwamba marekani bado itapendelea kupunguza wasi wasi kupitia mazungumzo yatakayohusisha pande zote.
Wakati huo huo Korea kaskazini imesema itaendelea kufanya majaribio ya silaha zake kila wakati na hatua yoyote ya kijeshi dhidi yake itazusha vita kamili , amesema afisa mwandamizi wa Korea kaskazini alipozungumza na BBC.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Grace Patricia Kabogo