1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Pence ajitosa kwenye kinyang'anyiro cha Ikulu ya White House

1 Juni 2023

Mike Pence anatarajiwa kutangaza rasmi kampeni yake ya kuwania urais kwa tiketi ya chama cha Republican na kumuweka katika kinyang'anyiro na bosi wake wa zamani, aliyekuwa rais Donald Trump.

USA Ehemaliger Vizepräsident Mike Pence
Aliyekuwa makamu wa rais wa Marekani Mike PencePicha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Jina la Pence linaongeza orodha ya wagombea takriban 10 wanaowania tiketi ya kupeperusha chama cha Republican katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024. 

Vyombo vya habari vya Marekani ikiwa ni pamoja na Associated Press na Reuters vimeripoti kwamba Mike Pence atazindua kampeni yake ya kutaka kuingia Ikulu ya White House mnamo Juni 7 katika jimbo la Iowa.

Vyombo hivyo vya habari vimenukuu vyanzo vinavyoifahamu vyema mipango ya makamu huyo wa rais wa zamani. Tarehe hiyo ya Juni 7 ambayo pia ni siku yake ya kuzaliwa, Pence anatarajiwa kutoa ujumbe kwa njia ya video kuelezea mipango yake kwa upana zaidi.

Uamuzi wa kuanza kampeni yake Iowa badala ya jimbo alilokulia la Indiana, unaonyesha jinsi timu yake ya kampeni ilivyolipa umuhimu jimbo hilo ambalo ni moja kati ya majimbo yanayopiga kura za mapema.

Soma pia: Ron DeSantis ajitosa katika kinyang'anyiro cha urais Marekani 2024

Timu yake ya kampeni inalichukulia jimbo la Iowa kama nguzo muhimu ya kuelekea kupata ushindi na anatumai kuwashawishi wapiga kura wengi Wakristo ambao wanaunda sehemu kubwa ya wapiga kura wa Republican katika jimbo hilo.

Pence ni mwanasiasa muhafidhina na ameonekana akipinga vikali haki za uavyaji mimba. Washauri wake wameeleza kuwa anapanga kufanya kampeni imara itakayompeleka katika kila pembe ya jimbo la Iowa.

Takriban wagombea 10 wa Republican wametangaza nia ya kuwania urais

Gavana wa Florida Ron DeSantis amezindua kampeni yake ya kuwania tiketi ya RepublicanPicha: Paul Hennessy/SOPA Images via ZUMA Press Wire/picture alliance

Wakati Pence sio mgeni kwa wapiga kura wafuasi wa Republican, washauri wake wanaamini kuwa anahitaji kujitambulisha tena kwao kwani wengi wanamfahamu tu kama makamu wa rais chini ya utawala wa Trump.

Miongoni mwa wanaowania tiketi ya chama cha Republican ni pamoja na gavana wa jimbo la Florida Ron DeSantis, ambaye anaonekana kuwa mpinzani mkubwa wa Trump. Gavana huyo tayari alitangaza kampeni yake wiki iliyopita.

Soma pia: Biden kuwania tena urais 2024

Orodha hiyo pia inawajumuisha wanasiasa wengine chungunzima akiwemo gavana wa zamani wa jimbo la New Jersey Chris Christie, seneta Tim Scott, aliyekuwa gavana wa Arkansas Asa Hutchison na mfanyibiashara Vivek Ramaswamy miongoni mwa wengine.

Christie, ambaye alikuwa mshauri wa Trump mnamo mwaka 2016 na baadaye kugeuka kuwa mkosoaji wake mkubwa, atazindua kampeni yake Juni 6.

"Ninamaanisha ninachokisema, na nasema ninachokiamini na hicho ndicho Marekani inahitaji kwa sasa."

Hata hivyo, kura za maoni za wagombea wa Republican zinaonyesha kuwa wapiga kura wengi bado wanampendelea Donald Trump huku akiwa na uungwaji mkono wa asilimia 53 wakati Pence ana asilimia 4 pekee.

Mgombea wa chama cha Republican atapambana dhidi ya mgombea wa Democrat ambaye wengi wanahisi atakuwa ni rais Joe Biden kwani tayari naye pia ametangaza nia ya kugombea tena urais.
 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW