1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pence kuzuru Mashariki ya Kati

Daniel Gakuba
15 Oktoba 2019

Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence ataanza ziara Mashariki ya Kati kuendeleza shinikizo dhidi ya Uturuki ili isitishe operesheni dhidi ya Wakurdi kaskazini mwa Syria. Ni baada ya Trump kuiwekea Uturuki vikwazo.

Polen Gedenken Zweiter Weltkrieg Warschau | Mike Pence
Mike Pence, Makamu wa Rais wa MarekaniPicha: Reuters/Agencja Gazeta/S. Kaminski

Katika mazungumzo na vyombo vya habari mjini Washington, Makamu Rais Mike Pence amesema Rais Donald Trump anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa kuyumba kwa usalama kwenye mpaka baina ya Uturuki na Syria, na amekanusha kwa mara nyingine, dhana kwamba Marekani iliiruhusu Uturuki kuanzisha operesheni dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi ambao siku za nyuma walikuwa washirika wa Marekani.

Amesema Trump alizungumza kwa simu na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, na kumweleza wazi kabisa, kuwa uvumilivu wa Marekani juu ya alichokiita ''uvamizi dhidi ya Syria'' umefika kwenye kikomo. Trump pia ameiwekea Uturuki vikwazo vipya, kuishinikiza kuacha operesheni hiyo ambayo inahofiwa yumkini ikalipa fursa nyingine kundi linalojiita Dola la Kiislamu kuanzisha tena uasi wake.

Mpango wa mabilioni ya dola mashakani

Vikwazo hivyo ni pamoja na kusitishwa kwa mazungumzo kuhusu mpango wa biashara baina ya Uturuki na Marekani wenye thamani ya dola bilioni 100, na ongezeko la asilimia 50 katika ushuru wa bidhaa za Uturuki zinazoingizwa Marekani.

Wanajeshi wa serikali ya Syria baada ya kufika karibu na mpaka baina ya nchi yao na UturukiPicha: picture alliance/AP Photo

Hali kadhalika, vikwazo hivyo vinawalenga maafisa watatu wa ngazi za juu wa Uturuki, pamoja na wizara za ulinzi na nishati za taifa hilo. Mike Pence amesema ikibidi, Marekani iko tayari kuongeza vikazo zaidi.

''Malengo ya rais yanaeleweka wazi, kwamba vikwazo vilivyowekwa leo vitaongezwa, ikiwa Uturuki haitasitisha mashambulizi mara moja, kuacha ghasia, na kukubali mazungumzo ya kutafuta suluhisho la kudumu katika mpaka baina yake na Syria.'' Amesema Pence.

Washirika wa Marekani, au magaidi?

Uturuki ilianzisha operesheni za kijeshi dhidi ya Wakurdi kaskazini mwa Syria Jumatano iliyopita, baada ya Marekani kuwaondoa wanajeshi wake katika eneo hilo.

Mapigano mapya yameuwa raia wengi kaskazini mwa Syria na kuwalazimisha wengine kuyakimbia makaazi yaoPicha: AFP/D. Souleiman

Kikosi cha Wakurdi hao kijulikanacho kama Syrian Democratic Forces, SDF ambacho siku za nyuma kilikuwa mshirika mkuu wa Marekani katika vita dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS kinachukuliwa na Uturuki kuwa kundi la kigaidi.

Mapigano baina ya pande hizo mbili yalichukuwa sura mpya mwanzoni mwa juma hili, baada ya SDF kupata makubaliano na serikali ya Syria mjini Damascus, ya kushirikiana kulinda mpaka baina ya Syria na Uturuki.

Makubaliano hayo ambayo yanaipa nguvu serikali ya Syria na Urusi ambayo ni mshirika wake mkubwa, yanazidisha wasiwasi miongoni mwa wakosoaji wa rais Donald Trump, kwa hoja kwamba yanadhihirisha kwamba kiongozi huyo wa Marekani alikurupuka katika uamuzi wake wa kuwaondoa wanajeshi katika eneo hilo.

ape, afpe

 

   

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW