Pence: Ubalozi wa Marekani kuhamishwa Jerusalem
22 Januari 2018Katika hotuba yake kwa bunge la Israel Knesset, Pence amesema utawala mjini Washington utaanza utekelezaji wa mipango ya kufungua ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem katika wiki za karibuni.
Makamu huyo wa rais wa Marekani amesema hatua ya kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel ni sawa sawa na kuutambua ukweli na kupingana na habari za kubuni, na siku zote ukweli ndio msingi mzuri wa kupatikana amani ya kudumu.
Hatua hii, ambayo ndiyo ya kwanza kabisaa kwa makamu wa rais alieko madarakani kulihutubia bunge la Knesset, imemulika nukta muhimu ya ziara ya siku tatu ya Pence nchini Israel, kusherehekea uamuzi wa rais Trump mwezi uliyopita kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.
Mike Pence alikaribishwa na kusifiwa na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Hata hivyo hatua hiyo imewakasirisha washirika wa Marekani kutoka nchi za kiarabu na wapalestina wenyewe ambao Pence hatokutana nao. Pence amesema yupo Israel kufikisha ujumbe unaosema kuwa Marekani inasimama pamoja na Israel.
Hata hivyo katika hotuba yake aliyoitoa ndani ya Knesset, Pence amewahimiza wapalestina kurejea katika meza ya mazungumzo na kuanzisha tena mazungumzo ya amani yaliyokwama kwa muda mrefu kati ya Palestina na Israel. Makamu huyo wa rais wa Marekani amesema nchi yake itaunga mkono hatua ya kuwa na madola mawili lakini itafanya hivyo iwapo pande zote mbili zitaridhia.
Rais wa mamlaka ya wapalestina atoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuitambua Palestina kama dola kamili
Akiizungumzia Iran Pence amesema Marekani haitokubali Iran kuwa na silaha za nyuklia. Amesema anatoa ahadi kwa Israel, mashariki ya kati na dunia kwamba Marekani haitokubali Iran kuwa na silaha za aina yoyote za nyuklia. Mike Pence Pia amesema Marekani itafanya kila iwezalo kuhakikisha inapunguza au kumaliza kabisa ugaidi duniani.
Wakati huo huo Rais wa mamlaka ya wapalestina Mahmood Abbas ameutolea mwito Umoja wa Ulaya kuitambua Palestina kama taifa. Abbas amesema wanautazama Umoja huo kama mshirika wa kweli na rafiki wa Palestina na kwahiyo wanawaomba wanachama wa Umoja huo kuitambua Palestina kama Dola. Rais Mahmood Abbas amesema hilo litawapa wapalestina matumaini ya kuwepo Amani.
Rais huyo wa Palestina ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada wa kifedha huku akiutaka kuwa na jukumu la kisiasa kuelekea Amani ya Mashariki ya kati. Abbas ameyazungumza hayo kuelekea mkutano wa Mawaziri wa Nchi za nje wa Umoja huo unaofanyika mjini Brussels.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga