Pendekezo la usitishwaji vita latolewa kwa Marekani na Iran
6 Aprili 2026
Shirika la habari la The Associated Press, limesema pendekezo hilo liliwasilishwa na wapatanishi kutoka Misri, Pakistan na Uturuki na lilitumwa usiku wa jana kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, pamoja na mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, Steve Witkoff.
Iran na Marekani bado hazijasema lolote juu ya pendekezo hilo.
Lakini afisa mmoja wa Iran ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa nchi hiyo haitoufungua Mlango-Bahari wa Hormuz kama sehemu ya makubaliano ya usitishwaji mapigano na wala haitokubali kuwekewa muda maalum wa kulipitia pendekezo hilo.
Ripoti hiyo ya mpango wa usitishwaji mapigano inajiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump, kutoa muda wa mwisho wa kesho Jumanne kwa Iran kuufungua mlango huo muhimu wa Hormuz au miundombinu yake ya nishati ishambuliwe vibaya.