Marekani imesema wanajeshi wake wako tayari kusalia nchini Iraq iwapo itakuwa tayari kushirikiana nao katika majukumu yasiyo ya kivita kwenye mapambano yake dhidi ya kundi la wanamgambo linalojiita Dola la Kiislamu, IS.
Matangazo
Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amesema hayo akiwa ziarani nchini Iraq hii leo kuelekea maadhimisho ya miaka 20 tangu Marekani ilipoivamia Iraq na kuuangusha utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Saddam Hussein.
"Wanajeshi wa Marekani wako tayari kubaki Iraq wakikaribishwa na serikali ya Iraq. Vikosi hivi vitashauri, vinasaidia na kuwezesha jukumu la kuunga mkono mapambano dhidi ya ugaidi yanayoongozwa na Iraq. Hii ni dhamira muhimu. Na tunajivunia kuunga mkono washirika wetu wa Iraq. Lakini lazima tuweze kushiriki kwa usalama ili kuiendeleza kazi hii muhimu," amesema Austin.
Austin ametoa kauli hiyo mbele ya waandishi wa habari baada ya mkutano wake na waziri mkuu wa Iraq Mohammed al-Sudani mjini Baghdad. Ziara hii ya kushtukiza ya Lloyd inafanyika ikiwa ni miaka 20 tangu muungano wa kijeshi ukioongozwa na Marekani ulipouangusha utawala wa Saddam Hussein, baada ya kulivamia taifa hilo kufuatia madai ya aliyekuwa rais George Bush kwamba Iraq ina hifadhi kubwa ya silaha za maangamizi.
Hatua hiyo ya kijeshi ya mwaka 2003 ilisababisha vifo vya maelfu ya raia wa Iraq na kusababisha ghasia ambazo kwa namna moja ama nyingine zilichangia kuibuka kwa kundi hilo linalojiita Dola la Kiislamu baada ya Marekani kuondoa wanajeshi wake mwaka 2011. Hata hivyo mwaka 2014, aliyekuwa rais Barack Obama alirejesha wanajeshi kuendeleza vita dhidi ya kundi hilo. Austin, ambaye ni afisa wa ngazi za juu zaidi katika serikali ya rais Joe Biden kuzuru Iraq, mwaka 2011 alikuwa mkuu wa vikosi vyote vya Marekani katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Waziri mkuu Sudani kwa upande wake alisema kwenye taarifa kwamba mbinu inayochukuliwa na serikali yake inalenga kudumisha uwiano katika suala zima lia ushirikiano wa kikanda na serikali za kimataifa kwa kuzingatia maslahi ya pamoja na kuheshimu uhuru na kwa maana hiyo utulivu wa Iraq ni suala la msingi zaidi kuelekea usalama wa ukanda mzima.
Marekani kwa sasa ina wanajeshi 2,500 nchini Iraq na wengine 900 nchini Syria wanaosaidia kwa kuyashauri majeshi ya mataifa hayo yanaopambana na kundi hilo la IS, ambalo mwaka 2014 liliyadhibiti maeneo makubwa kwenye mataifa hayo.
Lakini kwa upande mwingine ziara ya Austin inalenga kumsaidia Sudani kukabiliana na kuongezeka kwa ushawishi wa Iran nchini Iraq, hii ikiwa ni kulingana na afisa wa zamani wa Iraq na baadhi ya wafuatiliaji wa mambo.
Wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq mara kwa mara wamekuwa wakiwashambulia kwa maroketi wanajeshi wa Marekani na ubalozi wake mjini Baghdad. Mwaka 2020, Marekani na Iran al manusura ziingie kwenye mzozo kamili baada ya Marekani kumuua kamanda mkuu wa kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Iran Qassem Soleimani katika shambulio la ndege isiyotumia rubani.
Austin pia alitarajiwa kukutana na rais Nechirvan Barzani anayetawala mkoa wa Kurdistan nchini humo, katikati ya mzozo wa muda mrefu kati ya serikali ya kitaifa na ile ya kurdistan juu ya namna ya kushirikishana kwenye masuala ya bajeti na mapato yatokanayo na mafuta.
Tizama zaidi:
Mzozo wa kudumu — Miaka 40 tangu kuanza kwa vita vya Iran-Iraq
Vita vya Iran-Iraq ni mmoja ya mizozo mibaya zaidi ya kijesi ya Mashariki ya Kati. Mzozo huo uliodumu kwa miaka 8, ambamo silaha za kemikali zilitumiwa, uliua maelfu ya watu na kuigawa kanda kwa misingi ya madhehebu.
Picha: picture-alliance/Bildarchiv
Mabishano ya ardhi
Septemba 22, 1980, kiongozi wa Iraq Saddam Hussein alituma majeshi katika nchi jirani ya Iran, na kuanzisha vita mbaya iliyodumu kwa miaka minane ambamo maelfu ya watu waliuawa. Vita hiyo ilianzia kwenye mzozo juu ya ardhi kati ya mataifa hayo mawili yenye waumini wengi wa Kishia.
Picha: defapress
Mapatano ya Algiers
Miaka mitano kabla, mnamo Machi 1975, Hussein, wakati huo makamu wa rais wa Iraq, na Shah wa Iran walisaini makubaliano mjini Algiers kutatua mzozo wa mpakani. Baghdad hata hivyo, iliituhumu Tehran kwa kupanga njama ya mashambulizi na ikatoa wito wa kuondolewa watu kwenye visiwa viwili vya kimkakati katika njia ya bahari ya Hormuz, vilivyodaiwa na mataifa yote mawili pamoja na UAE.
Picha: Gemeinfrei
Chanzo muhimu cha maji
Septemba 17, 1980, Baghdad iliyatangaza makubaliano ya Algiers kuwa batili na ikadai udhibiti wa Shatt al-Arab yote - mto wenye urefu wa kilomita 200 unaotengenezwa kwa kukutana Tigris na Euphrates, ambayo inatiririka kwenye ghuba.
Picha: picture-alliance/AP Photo/N. al-Jurani
Mashambulizi ya bandari na miji
Vikosi vya Hussein vilishambulia viwanja vya ndege vya Iran kwa mabomu, kikiwemo cha Tehran, pamoja na miundombinu ya kijeshi na mitambo ya mafuta. Vikosi vya Iraq vilikumbana na upinzani mdogo katika wiki ya kwanza na viliteka miji ya Qasr-e Shirin na Mehran, pamoja na bandari ya kusini-magharibi mwa Iran ya Khorramshahr, ambako mto Shatt al-Arab unakutana na bahari.
Picha: picture-alliance/Bildarchiv
Adui wa pamoja
Mataifa mengi ya Kiarabu, zikiwemo Saudi Arabia na Kuwait, yaliiunga mkono Baghdad katika vita dhidi ya Iran, yakihofia kwamba mapinduzi ya Kiislamu yalioongozwa na Ayatollah Khomeini yangeweza kuwashawishi waumini wa Kishia katika Mashariki ya Kati. Mataifa ya Magharibi pia, yaliisaidia Baghdad na kuuza silaha kwa utawala wa Hussein.
Picha: Getty Images/Keystone
Iran yajibu mashambulizi
Mashambulizi ya kujibu ya Iran yaliishtua Iraq, baada ya Tehran kufanikiwa kurejesha udhibiti wa bandari ya Khorrramshahr. Baghdad ilitangaza kusitisha mapigano na kuondoa vikosi vyake, lakini Tehran ilikataa mpango huo na kuendelea kuishambulia miji ya Iraq. Kuanzia Aprili 1984, pande mbili zilishiriki "vita vya miji", ambamo miji ipatayo 30 kwa kila upande ilishambuliwa kwa makombora ya masafa.
Picha: picture-alliance/dpa/UPI
Silaha za kemikali
Moja ya matukio makuu ya vita vya Iran-Iraq lilikuwa matumizi ya Baghdad ya silaha za kemikali dhidi ya Iran. Tehran ilianza kutoa madai hayo 1984 - na kuthibitishwa na UN - na kisha tena mnamo 1988. Juni 1987, vikosi vya Iraq vilidondosha mabomu ya gesi katika mji wa Iran wa Sarasht. Machi 1988, Iran ilidai kwamba Baghdad ilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Iraq katika mji wa Halabja.
Picha: Fred Ernst/AP/picture-alliance
Mapatano
Julai 18, 1988, Khomeini alikubali azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kumaliza vita. Wakati idadi halisi ya waliouawa katika vita hiyo haijulikani, watu wasiopungua 650,000 walikufa wakati wa mzozo huo. Makubaliano ya kusitisha mapigano yalitangazwa Agosti 20, 1988.
Picha: Sassan Moayedi
Ukurasa mpya
Kuondolewa kwa utawala wa Hussein na Marekani mwaka 2003, kulianzisha zama mpya katika Mashariki ya Kati. Uhusiano kati ya Iraq na Iran umeboreka tangu wakati huo, na mataifa hayo mawili yanazidi kushirikiana katika nyanja za kiuhumi, kitamaduni na kijamii.