Peru yapata rais mpya wa tatu ndani ya wiki
18 Novemba 2020((Francisco Sagasti ameapishwa rais wa Peru katika kikao maalum cha bunge la nchi hiyo jana Jumanne.Rais Sagasi anabeba jukumu la kuutafutia ufumbizi mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo ya Amerika Kusini.
Francisco Sagasti mwenye umri wa miaka 76 ni rais wa tatu kuchaguliwa ndani ya wiki na siku chache nchini Peru na ni mwanasiasa kutoka chama cha siasa za mrengo wa wastani cha Morado na ameapishwa kuchukua madaraka kama kiongozi wa mpito hadi mwishoni mwa mwezi Julai mwaka 2021 ambapo atakuwa amekamilisha muhula wa rais aliyeondolewa madarakani na bunge Martin Vizcarra.
Kuondolewa madarakani kwa rais huyo Jumatatu iliyopita ndiko kulikosababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa katika taifa hilo. Itakumbukwa kwamba mrithi wake wa karibu aliyekuwa spika wa bunge Manuel Merino naye alilazimishwa kujiuzulu siku ya Jumapili siku kadhaa baada ya maandamano makubwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Maandamano
Maandamano hayo yalisababishwa na vifo vya watu wawili siku moja kabla. Rais wa mpito aliyechaguliwa sasa Sagasti aliomba radhi mara moja kwa niaba ya serikali kwa familia za waandamanaji hao vijana waliouwawa siku ya Jumamosi, wakiwa chini ya mikono ya polisi. Katika hotuba yake bungeni baada ya kuchaguliwa rais Sagasi alisema.
"Katika kipindi hiki cha mgogoro ambao haukuratajiwa na uliochochewa na majanga haya na matatizo yanayoikabili nchi yetu,uchumi,afya,masuala ya kijamii na matatizo ya kiusalama ni mambo ya msingi. Kuna haja kabisa ya kuweka utulivu, amani na kuondowa jazba.Lakini tafadhalini tusiyachukulie masuala hayo kama ni kuridhia,kukubali au kusalimu amri.Ni kinyume chake kabisa,tuyaangalia haya kama mwito wa kuchukua hatua,kujitolea sote wananchi wa Peru kwa nia njema kubadilisha hali hii na kuondokana na mgogoro huu''
Ahadi ya rais mpya
Raisi Sagasti ameahidi kuchukua hatua kadri inavyowezekana kupunguza kusambaa kwa janga la virusi vya Corona bila ya kuuathiri uchumi.
Maelfu ya Waperu walioingia mitaani kuandamana dhidi ya Merino,wameonesha kushusha pumzi kwa Sagasti kuingia madarakani.Waandamanaji waliingia mitaani kumpinga spika wa bunge Merino wakisema amefanya mapinduzi dhidi ya rais Vizcarra. Waandamanaji wanasema rais mpya Sagasti anabidi sasa kuchukua hatua ya kuonesha anailinda Demokrasia.
Ikumbukwe pia kwamba takribana nusu ya wabunge wa bunge la nchi hiyo wanakabiliwa na uchunguzi wa vitendo vya uhalifu na bunge hilo limepoteza umaarufu baada ya kumuondowa rais Vizcarra.
Mwandishi:Saumu mwasimba
Mhariri: Josephat Charo