Picha mpya za satelaiti El Fasher zaashiria mauaji makubwa
1 Novemba 2025
Picha mpya za satelaiti zinaonyesha kwamba mauaji ya watu wengi huenda yanaendelea ndani na nje ya jiji la Sudan la El-Fasher, siku chache baada ya mji huo kuangukia mikononi mwa wanamgambo wa RSF.
Ripoti ya Utafiti wa Misaada ya Kibinadamu ya Chuo Kikuu cha Yale iliyotolewa jana Ijumaa ilisema picha mpya zinawapa sababu ya kuamini kuwa idadi kubwa ya watu "wamekufa, kutekwa, au wamejificha".
Wanamgambo wa RSF ambao wamekuwa vitani na jeshi la nchi hiyo tangu Aprili 2023, waliudhibiti mji wa El-Fasher siku ya Jumapili, na kuliondoa jeshi nje ya ngome yake ya mwisho katika eneo la Darfur magharibi baada ya kuzingirwa kwa miezi 18.
Tangu kudhibitiwa kwa mji huo, kumeibuka ripoti za watu kunyongwa, unyanyasaji wa kijinsia, mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa misaada, uporaji na utekaji nyara, huku mawasiliano yakiendelea kukatika kwa kiasi kikubwa.