"Picha tofauti kabisa"
21 Mei 2007Mashambulio ya wikiendi iliyopita yanatoa sifa mbaya juu ya hali nchini Afghanistan ambayo ni tofauti na picha nzuri inayochorwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na wanasiasa. Hakuna eneo ambalo ni salama wala ni kweli kwamba majeshi ya nje yamewahi kuwashinda wanamgambo wa Taliban. Zaidi ni kinyume chake: Katika misikiti mingi ya nchi hiyo maimamu wanaita wazi wazi kuanzisha vita vya Jihad. Kila mwanamgambo mwingine wa Taliban anayeuawa atasababisha chuki zaidi.
Mfano mzuri ni kiongozi wa Taliban, Mullah Dadullah, aliyeuawa wiki moja iliyopita katika operesheni ya jeshi la Marekani. Katika maeneo mengi ya Afghanistan kumefanyika maombolezi , mengine ya siri au ya hadharani, kwa kiongozi huyu ambaye hata kati ya wenzake Waafghanistani alijulikana kuua watu kama mchinjaji. Kifo chake kilisababisha wafuasi wake kutaka kukilipiza kisasi. Kwa hiyo, kuna uwezekano mkubwa kuwa shambulio la Kundus au lile la Paktia ni la kulipiza kisasi kifo cha Mullah Dadullah.
Shambulio dhidi ya wanajeshi wa Ujerumani linazusha hofu kubwa. Tangu muda si mrefu, bunge la Ujerumani limekubali kutuma ndege za kivita Afghanistan kusaidia katika upelelezi wa anga. Maana yake ni kwamba zitasaidia kutafuta vituo vya maadui. Wataliban wanayajua hayo. Kwa hivyo, shambulio la Kundus pia litazusha mjadala mpya juu ya kupelekwa ndege hizo za chapa cha Tornado.
Licha ya kwamba vifo vya wanajeshi hawa vijana ni vibaya sana, haipaswi sana kuukosoa ujumbe mzima wa kijeshi nchini Afghanistan. Tangu kuanza shughuli yake, jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, limejitahidi hasa katika kujenga upya miundo mbino ya nchi hiyo iliyoathirika vibaya na vita. Na tayari kabla ya kutumwa ndege za Tornado, wanajeshi wa Ujerumani waliuawa katika mashambulio dhidi yao.
Mustakabali wa amani nchini Afghanistan utapatikana tu kupitia juhudi zaidi za kujenga upya nchi hiyo na kuendelea mkakati wa kuleta demokrasia kama ulivyoamuliwa kwenye mkutano wa Petersberg, Bonn. Ujenzi lakini unawezekana tu kufanyika katika maeneo yenye usalama. Kwa hivyo lazima majeshi ya ISAF yahakikishe usalama hata katika eneo la Kusini.
Kwa sasa hakuna njia nyingine ila tu mkakati huo wa pande mbili: Kwanza operesheni ya kijeshi dhidi ya Wataliban, na pili kujenga upya miundo mbino na kuupatia nguvu umma wa Afghanistan. Kindani lazima marekebisho yafanyike. Tatizo moja ni idadi kubwa ya raia wa kawaida wanaokufa na kujeruhiwa ambayo inaleta wasiwasi kati ya Waafghanistan juu ya uaminifu wa majeshi ya nje. Tatizo jingine ni kuwa idadi ya watu wanaonufaika kutokana na juhudi za ujenzi ni ndogo mno.
Ushindi katika vita dhidi ya Taliban utapatikana tu kwa kuungwa mkono na raia wa Afghanistan. Hapa kuna uhaba fulani. Inabidi kupata uungwaji mkono zaidi kutoka kwa Waafghanistan ili nchi hii isirudi tena katika enzi ya utawala wa kidikteta wa Wataliban. Baada ya kushindwa kuleta amani Iraq, kushindwa pia Afghanistan kungekuwa na athari kubwa hata nje ya mipaka ya nchi hiyo.